Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 5:03 am

NEWS: MUHIMBILI WAFUNGA MASHINE ZA KUSAFISHA DAMU

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine tatu za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, mashine hizo zinathamani ya TZS. 210 Mil na inatarajia kufunga mashine moja ya kusaidia mgonjwa kupumua (ventilator) yenye thamani ya TZS. 56 Mil katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ili kuhudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya virusi vya Corona.

Kwamujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma katika taasisi hiyo Aminiel Aligaesha imeeleza kuwa tayari wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa damu wameanza kuhudumiwa na wafanyakazi wa MNH waliopo Hospitali ya Amana tangu Ijumaa ya tarehe 24 Aprili, 2020 saa 12 asubuhi ambapo dawa na vitendanishi vya kutoa huduma ya kusafisha figo kwa sasa vinagharimiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Sambamba na hilo, Hospitali imefunga mtambo wa kuchuja maji (Portable RO) wenye thamani ya TZS. 28 Mil. na mtandao wenye miundombinu ya kusafirisha maji ili kuwezesha mashine hizo kufanya kazi ya kusafisha damu uliogharimu TZS. 12 Mil. Kutokanana hilo, MNH itapokea madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana kuanzia tarehe 28 Aprili, 2020 ili kujengewa uwezo kwenye Kitengo cha Kusafisha Damu pamoja na vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICUs) aina tano tofauti.

Aidha, MNH kupitia Hospitali ya Upanga na Mloganzila, ilipokea wagonjwa 93 kutoka Amana wakiwemo watoto wachanga 30 chini ya mwezi mmoja wakiwa na mama zao, watoto wanne chini ya miaka mitano, kina mama wajawazito 36, wagonjwa wa upasuaji 10 na wagonjwa 13 wenye magonjwa ya ndani (internal medicine).

MNH imekua bega kwa bega na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye maandalizi ya kupokea wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona katika Hospitali Rufaa ya Amana ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wagonjwa waliolazwa wanapata huduma. MNH inatoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kujinga na kuwakinga wengine kulingana na maelekezo yanayotolewa na Serikali.