Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:50 am

NEWS: MSEKWA AKIRI KUPOKEA MALALAMIKO YA KINANA NA MAKAMBA

Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, na Spika wa bunge Mstaafu wa Tanzania Pius Msekwa, amesema wamepokea Barua ya makatibu wa kuu wawili wastaafu wa ccm, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba ikiwa na malalamiko yao ya kukashifiwa dhidi ya Cyprian Musiba na kwamba madai yao hayo yatawasilishwa katika gazi ya juu ya chama hicho kwa ajili ya kujadiliwa.

Image result for pius msekwa

“Hii ni mara ya kwanza kupokea malalamiko ya aina hii, kwanza hakuna utaratibu wa kawaida, lakini tutafuata taratibu za chama, tutapeleka kwenye chama chenyewe.

Akizungumza jana na Muakilishi media kwa njia ya simu Spika Msekwa alisema tayari barua ya malalamiko ya wastaafu hao imewafikia na kwamba nyingine kama hiyo pia ilifikishwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu, Dk. Bashiru Ally.

“Barua hii nakala yake imeenda pia kwa Mwenyekiti wa chama na Katibu Mkuu. Hivyo sisi kama Baraza la Wazee tunasubiri utaratibu wa chama kwanza,” alisema Msekwa.

Katika hilo, Msekwa ambaye amepata pia kuwa Spika wa Bunge, alisema ushauri hautolewi kama amri bali unaombwa.

Akihojiwa jana na kipindi cha ‘Power Breakfast’ kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM, kuhusu ufafanuzi wa barua hiyo, Makamba alimtaka mtangazaji alisome tamko lao kwa sababu linajitosheleza.

“Soma hilo tamko linajitosheleza soma. Je, unalo? Hili tamko halifai kuondolewa koma wala nukta, linatakiwa libaki kama lilivyo, ni tamko refu, ni zuri, tumeliandika vizuri, tumeliandika mimi na rafiki yangu Kinana, halitakiwi kuongezwa kitu, libaki kama lilivyo,” alisema.

Alipoulizwa tamko hilo lina maana gani, Makamba alimwambia mtangazaji; “Wala usiulize, utakapolisoma utalielewa, mbona una haraka? Tafuta, usiwe na haraka.”

Baada ya majibishano hayo, mtangazaji huyo alimwuliza Makamba kama huwa wanaonana mara kwa mara na Kinana na alijibu; “Usitake tena maneno ya umbea kutoka kwangu soma tamko.”

Abdurahman Kinana, Yusuf Makamba ambao ni makatibu wakuu wastaafu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanahoji udhaifu uliokikumba chama cha CCM na serikali yake kwa kushindwa kulinda heshma yao na wananchi wengine kutokana na kuchafuliwa pia kudhalilishwa na Myu huyo anayejitambulisha kuwa ‘mtetezi wa Rais Magufuli

Makamba aliyehudumu nafasi hiyo kuanzia 2007-2011 na Kinana aliyehudumu kuanzia 2012-2018, Kufuatia kadhia hiyo, jana tarehe 14 Julai 2019 Mzee Makamba na Kinana wamemwandikia barua Mzee Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu la chama hicho, kumlalamikia kitendo cha Musiba kuwachafua viongozi wastaafu.

“Tuliamini kwamba pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu na huku mtu huyo akijinasibisha na serikali pamoja na rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma,” inaeleza sehemu ya tamko la Mzee Makamba na Kinana.

“Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawakuchukua hatua yoyote kuhusu jambo hilo. Na zaidi mtu huyu ameendelea kuwadhalilisha na kuvunjia heshima viongozi wastaafu na wengine katika jamii.”

"Kwa ushahidi wa kimazingira, Musiba anatumwa na wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na yeyote, zipo ishara wanaomkingia kifua wana mamlaka,baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalum, kwa watu maalum, kwa malengo maovu" - KINANA NA MAKAMBA

Mzee Kinana na Makamba wametoa tamko hilo, baada ya Musiba kuwatuhumu kwa zaidi ya mara mbili, kwamba wanahusika na vitendo vya kumkwamisha Rais John Magufuli kutekeleza majukumu yake.

“Kwa sasa Watanzania wote wanajua kuwa haya anayosema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali siyo ya kwake, yeye anatumwa kutekeleza maagizo tu na kutumika kama kipaza sauti.Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu, katika mazingira hayo hatuwezi kukaa kimya,” wamesema.

“Tunasikitika kwamba Musiba licha ya kuwatuhumu na kuwakashifu Watanzania wenzake viongozi na watendaji wa serikali, ameachwa akitamba jambo linaloashiria kwamba anakingiwa kifua , hata anapotumia lugha za vitisho na za kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake,” wamesema.

Makatibu hao wastaafu wa CCM wamesema wamechukua hatua hiyo badala ya kwenda mahakamani, ili wazee wa CCM watumie busara zao katika kushughulikia jambo hilo. “Tunafanya hivyo kwa kuzingatia katiba ya CCM , tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja mshikamano na utulivu ndani ya chama na nchi,” walisema