Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 10:31 am

NEWS: MPINZANI SRI LANKA ASHINDA KITI CHA URAIS

Tume ya Uchaguzi nchini Sri Lanka imemtangaza mgombea wa upinzani na waziri wa zamani wa ulinzi, Gotabaya Rajapaksa, kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata zaidi ya asilimia 50. Gotabaya, luteni kanali mstaafu mwenye umri wa miaka 70, alipata asilimia 52.2 ya kura kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.

Sajith Premadasa, waziri mwenye msimamo wa wastani, ameshindwa kwenye uchaguzi wa rais wa Sri Lanka.

Mpinzani wake mkuu miongoni mwa wagombea 35 alijikingia asilimia 41.99, Sajith Premadasa - waziri wa serikali inayomaliza muda wake na mwenye msimamo wa wastani - alitangaza mapema kukubaliana na matokeo hayo na kumpongeza Gotabaya.

Idadi ya waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 83.7 ya watu waliosajiliwa kwa ajili ya uchaguzi huu, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

Ambapo Premadasa alikuwa na uungwaji mkono mkubwa kwenye maeneo yanayokaliwa na Watamil, mwenzake Gotabaya alikuwa akiungwa mkono na maeneo yanayokaliwa na jamii ya Sinhalese, ambao ndio wengi nchini Sri Lanka

Gotabaya anatazamiwa kuapishwa siku ya Jumatatu (18 Novemba).

Sri Lanka Wahl 2019 | Gotabaya Rajapaksa, Kandidat SLPP (picture-alliance/Zuma Press/P. Dambarage)

Ushindi unaoleta kumbukumbu za kutisha

Gotabaya, aliyepewa jina la utani la "Terminator" na familia yake mwenyewe kutokana na kusimamia operesheni ya kikatili kabisa dhidi ya kundi la waasi

la Tamil Tigers miaka 10 iliyopita, ametangazwa mshindi ikiwa ni miezi saba tu tangu mashambulizi ya wapiganaji wenye itikadi kali kuwauwa watu 269 nchini humo.

Kaka huyo wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Mahinda Rajapaksa, alitumia kampeni yake kuzungumzia juu ya masuala ya usalama, akiapa kuyaangamiza makundi ya itikadi kali ndani ya taifa hilo lenye waumini wengi zaidi wa dini ya Buddha, kufuatia mashambulizi hayo ya tarehe 21 Aprili, ambayo yanaaminika kufanywa na kundi la ndani la siasa kali za kidini.

Ushindi huu, hata hivyo, unatajwa kupokelewa kwa mashaka na jamii za wachache nchini Sri Lanka, wakiwemo Waislamu na Watamil, na pia waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binaadamu na jumuiya ya kimataifa wanaokumbuka jinsi miaka kumi ya utawala wa kaka yake, Mahinda, kuanzia 2005 hadi 2015 kilivyokuwa cha kigumu kwa makundi hayo.

Ndugu hao wawili, Mahinda na Gotabaya, waliendesha operesheni yenye mafanikio makubwa iliyokomesha miaka 37 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na Watamil waliokuwa wakipigania kujitenga na kuunda taifa lao.

Muongo huo mmoja unakumbukwa na wengi kama kipindi cha uvunjwaji wa haki za binaadamu, mauaji ya kiholela na pia cha kujikurubisha sana na China.