Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:38 am

NEWS: MO DEWJI ANYANG'ANYWA MASHAMBA 6 NA SEREKALI

Dar es Salaam: Sereli kupitia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula jana Jumatatu ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuyafuta umiliki mashamba sita yenye ukubwa wa ekari 12, 915. 126 ya Bilionea namba moja nchini Mohammed Dewji maarufu kama 'MO' kupitia kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL ) yaliyopo Korogwe jijini Tanga.

Kwa Mujibu wa Taarifa ilitolewa kwa umma na kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo imesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo umefikiwa baada ya mapendekezo yaliyotolewa na halmashauri ya wilaya ya Korogwe kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu.

Imesema mapendekezo hayo yaliwasilishwa kwa Rais John Magufuli na wizara kwa nia ya kufutwa mashamba hayo ya MeTL ambayo ofisa mtendaji mkuu wake ni bilionea namba moja kijana barani Afrika, Mohammed Dewji ‘Mo.’ Mashamba yaliyofutwa ni yale yaliyopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge wilayani Korogwe.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo, Mabula amesema mashamba yaliyobatilishwa ni kati ya mashamba 14 yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises,eneo la Mazinde wilayani Korogwe.

Amesema uamuzi huo unalenga kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za Serikali kuzingatia masharti ya uwekezaji. Amesema mara baada ya halmashauri ya wilaya ya Korogwe kupeleka mapendekezo ya kufutwa mashamba ya Mohammed Enterprises, wizara ya ardhi ilifanya ufuatiliaji katika halmashauri husika kuhusu kutoendelezwa mashamba na baada ya kujiridhisha ikawasilisha maombi hayo kwa Rais na kuridhiwa.

Mabula amesema uamuzi huo wa Rais kuridhia ubatilishaji mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises unalenga kuhakikisha wote waliopewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanazingatia masharti na taratibu za uwekezaji. Naibu waziri huyo amesema mashamba ambayo hayajabatilishwa yamewekewa utaratibu kwa nia ya kuyaboresha kwa kuwa baadhi yake yanahitaji maboresho kwa nia ya kufanya vizuri.