Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 1:44 pm

NEWS: MNYIKA AITAKA SEREKALI ITOE MAELEZO USITISHWAJI BOMBA LA GESI

Dar es salaam: Mbunge wa Kibamba John Mnyika (Chadema), ameitaka serekali kutoa maelezo kuhusu usitishwaji wa mradi wa bomba la gesi na badala yake kuhamia kwenye mradi wa Umeme wa Stieglers Gorge unakadiriwa kugharimu dola za kimarekani bilioni 2.9 ambayo ni sawa na takribani shilingi trilion 6.5 za kitanzania. (Anaandika Issa Deyssa)

"Sehemu kubwa ya Bomba la gesi lililojengwa kwa zaidi ya TZS trilioni 2 haitumiki mpaka sasa, tunaitaka Serikali ya Magufuli itueleze ni kwanini iliachana na mradi wa gesi na ikaanza kuzungumza mradi wa Stieglers na mikataba ya ujenzi wa bomba hilo iletwe bungeni" amesema Mnyika

Akiongea na Waandishi wa Habari leo Jumapili Mei 26, 2019 Mnyika amesema Serikali inalazimika kuwatoa kafara wananchi wake na inabidi ichukue hatua ya kupunguza kiwango cha fedha kwenye miradi mingine inayowagusa wananchi wa kawaida kama maji, afya na elimu ili fedha hizo zielekezwe kwenye mradi wa Stieglers.

Mnyika amehoji juu ya Utekelezaji wa Mradi huu, akisema kuwa Wachambuzi wa Wizara ya Nishati na Madini wakati Rais Jakaya Kikwete walisema mradi huu ikiwa utafanyika, basi huenda utakamikika baada ya miaka 12, lakini Serekali chini ya Rais Magufuli umesema utakamilisha mradi huu kwa kipindi cha miaka mitatu tu.

"Wachambuzi wa Wizara ya Nishati na Madini wakati ule walisema mradi huu utakamikika baada ya miaka 12, Sasa ni miujiza gani ambayo Serikali ya Rais Magufuli inataka kufanya ili mradi wa Stiegler's ukamilike kwa miaka mitatu?" amehoji Mnyika

Mradi wa Umeme wa Stieglers Gorge ulitiliwa saini Mwezi Desemba tarehe 12 mwaka jana chini ya Rais Magufuli aliweka saini na wakandarasi wa mradi huo kutoka Misri wakiwa pamoja na waziri mkuu wa nchi yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Misri Tanzania, Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa

Hatua hiyo inakuja baada ya miaka 40 tangu utafiti wa uzalishaji wa umeme kutoka mto Rufiji ambao unaweza kuzalisha megawati 2,100 kufanyika wakati huo Tanzania ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa na fedha za watanzania wenyewe kwa kiwango cha dola za kimarekani bilioni 2.9 ambayo ni sawa na takribani shilingi trilion 6.5 za kitanzania.

"Mradi huu utatumia fedha kidogo kuliko vyanzo vingine vya umeme, Uniti moja inayozalishwa na umeme wa maji ni shilingi 36 na huku umeme unaotengenezwa na nyukilia ni shilingi 65 kwa uniti moja wakati umeme wa jua ni shilingi 103.05 , upepo ni shilingi 103.05, makaa ya mawe ni shilingi 118, Gesi asilia shilingi 147 na mafuta shilingi 426 kwa uniti moja. Hivyo utofauti ni mkubwa sana kati ya maji na vyanzo vingine" alisema Rais Magufuli .