Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:46 am

NEWS: MKURUNGEZI WA MANISPAA YA DOM ATANGAZA KIAMA KWA WAMILIKI WA VIWANJA

DODOMA: MKURUNGEZI wa halmashauri ya manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ametangaza kiama kwa wamiliki wenye viwanja vikubwa ambao wameshindwa kuviendeleza kwa zaidi ya miaka mitatu na kuvirudisha kwa wananchi wanyonge.

Mbali na hilo ametangaza kutoa viwanja vya wananchi ambao walipewa barua za umiliki wa viwanja lakini hawajaweza kuziendeleza mpaka sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Kunambi amesema wamiliki wote wenye viwanja vikubwa na zaidi ya kimoja wamepewa muda wa siku 90 tangu sasa wawe wameisha endeleza vinginevyo viwaja hivyo vitatwaliwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi.

Kwa wale ambao walipewa barua ya viwanja lakini hawajafanya malipo nao wamepewa muda wa siku 30 kuanzia sasa vinginevyo viwanja hivyo vitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Kunambi ambaye ameonekana kujitapa katika utendaji wake wa kazi tangu kuvunjwa kwa iliyokuwa Mamlaka ya ustawishaji Makao Makuu (CDA) amesema kuwa hakuna mtu hata mmoja ambaye ataonewa katika kutekeleza suala zima na upangaji wa mji wa Dodoma.

Licha ya wananchi wa Dodoma kufurahishwa na serikali kuivunja CDA kwa kile ambacho kilionekana kuwa kero kwa kuvunjiwa lakini bado Mkurugenzi wa Manispaa ambaye amepewa majukumu ya CDA kutangaza kuwa wale wote ambao wamejenga kiholela watavunjiwa nyumba zao.

Kunambi akiendelea kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari amesema wananchi wote ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu maeno hayo yatachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kupewa watu ambao ni wahitaji wa viwanja.

Akizungumzia kuhusu wageni ambao wamekuwa wakinunua viwanja kwa madalali, Kunambi amewataka wateja wote wanaotaka kununua viwanja wafike katika ofisi ya mkurugenzi ili kupata viwanja vya uhakika kwani wasipofanya hivyo watatapeliwa.

Akizungumzia kitendo cha Manispaa kukusanya mapato na kuvuka lengo amesema katika mwaka wa fedha 2016/17 wamevuka lengo na kufikia asilimia 17.