Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:50 am

NEWS: MISWADA YA SHERIA BADO NI GUMZO BUNGENI

DODOMA: KAMATI ya Bunge ya pamoja iliyoundwa na Spika Job Ndugai ya kujadili miswada mitatu ya Ulinzi na Raslimali za Nchi imeendelea kupokea maoni ya Wadau huku wadau hao wakishauri Sheria zinazotungwa ziwe na manufaa kwa Taifa.

Miswada iliyowasilishwa hivi karibuni bungeni ni ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali zenye upungufu wa mwaka 2017,Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti hasi katika Mikataba ya Maliasili wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusina na Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017.

Katika kikao hicho kilichofanyika jana katika ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Mkoani hapa kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Dotto Biteko na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria Mohamed Mchengerwa.

Waliohudhuria Kikao hicho ni Mawaziri,Wabunge na Wadau mbalimbali ambao walipata nafasi ya kuchangia.

DK. NSHALA

Wa kwanza kutoa maoni alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk.Rugemeleza Nshala ambaye alisema kuwa kuna ulazima wa kuzungumzia kuhusu mikataba ya pande mbili au pande tatu ambazo nchi itaingia.

“Kuhusu migogoro ya kiuwekezaji ikatatuliwe mahakama za nje hapo ndo kuna tatizo kwa hiyo inabidi kiondolewe hicho kipengele na tuseme mikataba yote ya pande mbili au tatu zinazoendelea kama inakiuka uwezo wa mahakama zetu kuweza kuamua migogoro hii mikataba ni batili naomba lizingatiwe,”alisema

Alisema kuna muswada unatoa nafasi kwa serikali kuweza kujadiliana lakini wao kama taasisi wanaona ni lazima muswada ueleze ni nani ataingia kwenye majadiliano hayo huku akitaka sheria iseme wazi.

“Kama bunge limetoa azimio kwamba mikataba hiyo ijadiliwe sasa wakati serikali na wachukuaji wanajadiliana wakashindwa kukubaliana wanakwenda wapi?, sheria inasema kwamba hivyo vipengele kama havijakubalika haviendelei tena,tuseme kama hatujakubaliana twende mahakamani,”alisema Mkurugenzi huyo

Alisema Mahakama za hapa nchini ndio ziamue hivyo vipengele ambavyo vitaonekana vinakinzana na kuagiza mgogoro labda umalizike ndani ya muda fulani na kama vipengele hivyo ni vya msingi au sio vya msingi.

Akizungumzia kuhusu kuundwa kwa Kamisheni ya madini, Mkurugenzi huyo alisema kuondoa madaraka ya Waziri kujadiliana kwenye mikataba lakini kuna dhana ambayo ipo ya mikataba kujadiliwa lakini sheria haisemi ni nani ambaye atajadili.

“Haisemi ni Waziri gani na taasisi gani ya serikali ambayo itaanzisha majadiliano au kama ni Kamisheni ya madini ndiyo itapatiwa madaraka hayo sheria haisemi,”alisema

Pia Dk. Nshala alisema kama Kamisheni haina utaalam huo ni namna gani itakuwa na utaalamu kwa kuwa na timu ya wataalamu kuweza kujadiliana.

“Kama tunaona kuna tatizo kuwa na mikataba sisi tunaona kwamba kwanini tusifuate mfano wa Zambia na Afrika kusini ambapo utaratibu wao unasema hakuna kujadiliana mambo ya mikataba wameingiza kwenye sheria ambapo ukitaka leseni ya kuchimba madini omba leseni na masharti yake yatakuwa kwenye sheria,”alisema Mwanasheria huyo

Alibainisha hakutakuwa na masuala ya kumuweka mtu sawa hivyo mtu atatakiwa kufuata masharti yaliyowekwa kwenye matakwa ya sheria.

“Ni vyema sisi kama tunaona hatuna utaalam wa kujadiliana haya na kufikia uwezo wa Botswana sisi tufuate leseni, Afrika kusini walitaka kufanya kuwa na mikataba wakakataa kwamba mtu ataomba leseni na kukutana na masharti ya kisheria humo na sio kuingia mikataba, tuangalie uwezekano wa hicho kitu tusitake kuinyanyasa serikali,”alisema

Vilevile, alisema sheria hizo hazizungumzii namna ya kujitoa kwenye hiyo mikataba lazima iseme serikali itaingia kwenye mchakato wa kujitoa katika mikataba ambayo inaibana.

“Kwanini serikali isihakikishe hatuwezi kusaini kujifunga na mambo ya migogoro kutatuliwa kwenye mahakama za kimataifa kwa kuwa kutakuwa na political risk hapa, maana watatupeleka nje na wakishinda wataenda kuchukua fedha MIGA inatakiwa ilipe na itakuja hapa kudai nchi ilipe tunabidi tujitoe kwa kuwa ni hatari sana, ”alisema

MWAKILISHI WA WAWEKEZAJI WAKUBWA

Kwa upande wake,Mwakilishi kutoka Tanzania Chamber of Minerals, Gerald Mturi ambaye alitoa maoni kwa niaba ya Wawekezaji Wakubwa alidai kuwa katika mchakato wa kusafirisha madini nje ya nchi kuna mambo hajawekwa sawa ni nani atawajibika kama utatokea upotevu na mwekezaji na atafidiwaje.

Kuhusu migogoro kutatuliwa kwenye mahakama za hapa nchini, Mturi alisema suala la mashauri yote kujadiliwa nchini kitawapa shida wawekezaji.

“Wawekezaji wa nje kwa utaratibu huo hauleti amani, suala hili linatakiwa kuangaliwa upya kwa kuwa tutawakimbiza wawekezaji,”alisema

Aidha Mturi alisema katika kifungu 10(1)-(3) kinachosema kwamba serikali inaweza kuwa na asilimia 50 ya hisa kwenye mgodi na kampuni ikatakiwa kupelekea tena hisa 30 kwenye soko la hisa jambo ambalo litaifanya kampuni kubaki na asilimia 20.

“Sisi tunapendekeza kipengele hicho mfikirie namna ya kukiondoa hasa cha upelekaji hisa asilimia 30 kwenye soko la hisa kwa kuwa kitakimbiza wawekezaji,”alisema Mturi

BASHE ACHARUKA

Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Mjini,Hussein Bashe alimbana mwakilishi wa Wawekezaji Wakubwa, Mturi, kuwa amehusika na kudhulumu fedha za tozo za ushuru katika Halmashauri ya Nzega.

‘’Tunasema tukiweka kila kitu katika sheria tutakimbiza Wawekezaji Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982, ilisema kuwe na Service Levy ya asilimia 0.03 wewe umeondoka Nzega bila ya kulipa,haujalipa umelipa ‘only’ 2 Bilioni kwa hoja kwamba kulikuwa hakuna ‘by law’ ndio maana tunasema kila kitu kiwekwe kwenye sheria’’

‘’Ameongelea Nchi kama Botwana wana Miundombinu mizuri lakini hajasema katika kikao hichi ana Share Holder ya asilimia 40 kwenye Migodi hiyo’’

‘’Pia nataka nitoe mfano ukienda Nyamongo kwa Heche(John) Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka Polisi inaweka nini wanalipwa hawa, hivyo ‘Depositi’ iliyopo chini ardhi unayoenda kukopea ndio msingi wa wewe kukopa kwanini unadhani wewe ni vibaya kwa Serikali kwamba wewe unakuja na Teknolojia na mtaji mimi nina Maliasili kwanini ni vibaya’’aliuliza Bashe

Akijibu,Mtuly alisema suala la ushuru katika Halmashauri ya Nzega lipo kisheria kwa sababu kuna Sheria ya Locol Government Finance ambayo haiwezi kusimama yenyewe kwani hiyo sheria inaziruhusu Halmashauri kutoza mpaka asilimia 0.03.

MWAKILISHI WA WACHIMBAJI WADOGO

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Wachimba Madini Wadogo wadogo Tanzania,John Bina akitoa maoni kwa niaba ya wachimbaji wadogo wadogo alishauri Madini ya Tanzanite yawe na Sheria maalum kutokana na kupatikana Tanzania pekee.

‘’Katima Miswada yote mitatu hakuna sehemu inayohusu Wachimbaji wadogo wadogo lakini muda wa umiliki tunapewa miaka saba pekee hili liangaliwe’’alisema

CWT

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT),Alfonce Mbasa alisema Miswada hiyo isifanywe kidharura kwani hata ile ya mwanzo ilikuwa na makosa sababu ya kufanywa kidharura.

‘’Miswada isifanywe kidharura kwani hata ile ya mwanzo ilikuwa na makosa kama hayo lazima ijadiliwe,tukae na wanasheria watuelekeze kifungu kwa kifungu kisha tupeleke kwa wananchi nao waujadili sasa sisi tunataka haraka haraka tu’’alisema Mbasa.