Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:25 am

NEWS: MIMBA KWA WANANFUNZI WAMPA UGUMU WA KAZI MWANASHERIA

MOROGORO: Mwanasheria Grace Timoth ameiomba Serikali kuruhusu kesi zinazohusu mimba kwa wanafunzi, kuendeshwa na mahakama za mwanzo, badala ya mahakama za wilaya.

Amesema hali hiyo itawaondolea mzigo wazazi na mashahidi kufika kwenye mahakama za wilaya. Amesema kwa sasa watu wengi wamekuwa wakishindwa kufika wilayani, hali inayosababisha kesi nyingi kushindwa kupata ushahidi wa kutosha, hivyo watuhumiwa kuachiwa huru.

Timoth alitoa ombi hilo hivi karibuni wakati wa mafunzo kwa wenyeviti na wajumbe wa bodi za shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Mafunzo hayo yaliandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali, inayojihusisha na masuala ya utawala bora ya Jikwamue Development Association (JIDA).

Mafunzo hayo yaliendeshwa kutokana na wilaya hiyo, kukabiliwa na tatizo la mimba, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2016/2017 wanafunzi 49 wamepata mimba. Mratibu wa Mradi wa Elimudira wa asasi ya JIDA, Shaban Chande alisema elimu itakayotolewa kwa wazazi kupitia mradi huo kwa ufadhili wa taasisi ya The Foundation For Civil Society kwa miezi sita, italeta hamasa ya uchangiaji chakula kwa wanafunzi shuleni.

Alisema elimu hiyo itahamasisha wazazi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na hosteli za kuishi wanafunzi hasa wa kike, badala ya kupanga mitaani, ambako wamekuwa wakikosa uangalizi wa wazazi.