Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 5:39 pm

NEWS: MHE.MTATURU AISHUKURU SERIKALI KWA KUTOA FEDHA KUKAMILISHA JENGO LA ZAHANATI ULYAMPITI.

SINGIDA: Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mhe. Miraji Mtaturu amemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa Fedha kiasi cha shilingi milioni 154 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ulyampiti Wilayani Ikungi.


Ukamilikaji wa Zahanati hiyo utaondoa adha waliyokuwa wanaipata wananchi ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo Ikungi, Itigi na wengine kwenda Mkoani Singida.


Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ulyampiti Mhe. Mtaturu ametoa shukrani zake kwa serikali kwa kutimiza ahadi yake ndani ya muda mfupi.


"Mwishoni mwa mwaka 2018 Makamu wa Rais alipofanya ziara wilayani Ikungi wakati huo nikiwa mkuu wa wilaya aliona changamoto waliyokuwa wanaipata wananchi wa kijiji cha Ulyampiti ,na kupitia ziara hiyo nilimuomba mbele ya wananchi asaidie fedha za umaliziaji ujenzi wa Jengo la Zahanati hiyo ili kuweka karibu huduma ya Mama wajawazito, watoto wadogo na Wazee na nashukuru ombi hilo lilishatimizwa na jengo limekamilika,"alisema Mtaturu.


Amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt John Magufuli kama ambavyo amefanya yeye kuleta fedha za zahanati hiyo ambayo imeanza kutoa huduma kwa wananchi.


Amesema ili kuonyesha shukrani kwake washiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuchagua viongozi watakao baini na kufuatilia kwa ukaribu shughuli za maendeleo na sio viongozi wa kujaza nafasi.