Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 12:49 pm

NEWS: MHE MTATURU ACHANGIA SH MIL 8.8 KWA AJILI YA MIUNDOMBINU KATIKA SHULE YA SEKONDARI IKUNGI.

SINGIDA: Mbunge wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu ameshiriki mahafali ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Ikungi na kuchangia Sh Milioni 8.8 kwa ajili ya umaliziaji wa jengo la Maabara lililopo shuleni hapo.


Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya mifuko 30 ya Saruji yenye thamani ya Sh 480,000 na Mbao za upauaji kwa ajili ya jengo la Maabara lenye vyumba vitatu zenye thamani ya Sh Milioni 8.4.


Akizungumza katika mahafali hayo Mhe Mtaturu ameipongeza Jumuiya ya shule kwa juhudi zao za kusimamia taaluma.


"Niwahakikishie kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia kama ilivyo dhamira ya Rais wetu Mhe Dk John Magufuli,


"Mimi mbunge nitaendelea kuunga mkono maendeleo kwenye jimbo na wilaya kwa ujumla ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya utoaji wa elimu,najua maendeleo yoyote yanaanzia kwenye elimu,hivyo ni lazima tuwekeze katika elimu,"alisema Mhe Mtaturu.


Ili kutilia mkazo jambo hilo amewahamasisha wanafunzi wa kidato cha nne kusoma kwa bidii na kuahidi kutoa Sh laki moja kwa mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza na elfu 20 kwa mwanafunzi atakayepata daraja la pili ikiwa ni kampeni ya kuongeza ufaulu.


Katika kuunga mkono juhudi za Mbunge,Wazazi na Walezi waliohudhuria mahafali hayo walihamasika na juhudi hizo na kuchangia Sh 350,000/=,viti na meza sita.

Akisoma taarifa ya shule,Mkuu wa shuke hiyo Order Fabian alieleza changamoto zilizopo shuleni hapo kuwa ni pamoja na utoro wa wanafunzi,ukosefu wa maabara na upungufu wa wafanyakazi wasio walimu.


"Shule yetu ina kidato cha tano na sita ikiwa na wanafunzi 720,pamoja na changamoto hizo pia kuna mwamko mdogo wa wazazi na jamii kuhusu elimu kwa watoto,hatuna huduma ya maji hali inayosababisha usumbufu kwa wanafunzi wa bweni,”alisema mwalimu huyo.


Pamoja na changamoto hizo aliweka bayana jitihada zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanapandisha ufaulu.

“Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dokta John Magufuli kwa kuleta elimu bila malipo ambayo naomba nikiri kuwa imewapa fursa watoto wote kupata elimu,”alisema mwalimu mkuu huyo.


Aidha amesema upande wa huduma ya maji Mhe Rais Magufuli ameshatoa Sh Bilioni 2 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji ambapo miongoni mwa visima 28 vitakavyochimbwa kimoja kitachimbwa karibu na shule hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule Shaban Mukhandi amemshukuru mbunge Mtaturu kwa jitihada zake za kuhamasisha maendeleo wilayani humo.


“Tangu ukiwa Mkuu wa Wilaya umekuwa pamoja na sisi,pamoja na majukumu uliyonayo lakini upon a sisi,tuna imani kwa sasa umekuwa mbunge utasaidia kuwasemea wananchi serikalini ili kutatua changamoto tulizonazo,

“Hili jengo la maabara ni kielelezo tosha cha juhudi zako za kuhamasisha maendeleo,lilitelekezwa kwa miaka 9 lakini chini ya uongozi wako umelifufua na kwa sasa limefikia hatua ya kupaua,”alisema Mwenyekiti huyo.