Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 1:24 pm

NEWS: MHE MTATURU ACHANGIA MILIONI 6 KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE YA MANKUMBI NA SIMBIKWA.

SINGIDA; Mbunge wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu amechangia sh milioni 6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi ya Mankumbi na Simbikwa huku akiiasa jamii kushirikiana na serikali katika kuhakikisha shule hizo zinakamilika.


Ukamilikaji wa shule hizo utaondoa adha kwa wanafunzi ya kutembea umbali mrefu wa kilomita 12.

Akizungumza octoba 18 akiwa kata ya Kikio katika muendelezo wa ziara zake jimboni humo,Mhe Mtaturu amesema serikali imefanya kazi nzuri ya kutoa elimu bila ya malipo hivyo wao hawapaswi kuwa vikwazo wa kuwakosesha watoto kupata huduma hiyo.


“Najua namna mlivyo na hamu ya kuwa na shule yenu,najua namna mlivyowahurumia watoto wetu,najua namna watoto walivyoteseka kuvuka mto wakati wakienda na kurudi shuleni hasa wakati wa mvua,wakati nikiwa mkuu wa wilaya nilisisitiza tuhakikishe shule inaanzishwa,


“Mimi kama mwakilishi wenu sitokubali kuona shule hii haianzi,kamwe sitakubali,ninachomuomba mkurugenzi wa halmashauri ahakikishe kwamba tunafanya utaratibu unaowezekana kuhakikisha watoto wa darasa la kwanza hadi la nne wanasoma hapa,kwa sababu watoto hawa ni wadogo hatuwezi kuwaruhusu watembee umbali mrefu,na ili kusukuma hili mbele nachangia milioni 6 kwa shule hizi mbili”alisema Mhe Mtaturu.


Amesema Rais Dk John Magufuli ametoa elimu bila ya malipo hivyo hawapaswi kuwakwamisha watoto hao kwa namna yoyote kupata elimu hiyo.

“Nimekuwa na taarifa kuna viongozi wa kijiji hiki wamekuwa wakikwamisha shule hii isianze lakini nataka niwaambie huyo kiongozi hata kama ni upinzani elimu ya mtoto ni muhimu kuliko chama,huu ni uuaji kwa sababu mtoto bila elimu unamuua ,


“Leo hii tunasema elimu kwa wote hata kwenye katiba imetajwa lakini kiongozi anapewa dhamana hataki kushiriki shughuli za maendeleo,najua diwani hajawahi kuja hapa na hashiriki kwenye jambo hili ,sasa naomba niwaambie nikiwa mbunge wenu nitasimama na nyie kuhakikisha shule hizi zinakuwa tayari na nitaendelea kuunga mkono juhudi za Rais wetu za kutoa elimu elimu bila ya malipo,”alisema mbunge huyo.

Ili kutekeleza hilo ameahidi kuhakikisha miundombinu ya shule inakamilika ikiwa ni pamoja na kupeleka walimu na hivyo kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira rafiki ili nao wajione kuwa ni tunu katika Taifa hili.

“Tunataka watoto hawa wasisononeke wakahisi sisi wazazi tumeshindwa kuwaandalia mazingira ya wao kupata elimu,niwaombe muendelee kutoa nguvu kazi kama kuleta mchanga,maji na mawe ili hizi fedha nilizotoa zinunue vifaa vya madukani,


“Katika uwakilishi wangu kwenu nimekuja na kauli mbiu ya maneno kidogo kazi zaidi hapa kazi tu,najua hamtaki maneno tena mnataka vitendo,hivyo niwaahidi kwangu mtaona maneno kidogo ila kazi zaidi,tushirikiane,”alisisitiza Mhe Mtaturu.

Amemshukuru Rais Dk Magufuli kwa kupeleka Sh Milioni 451 kila mwaka wilayani Ikungi kwa ajili ya kugharamia elimu bure.

Amewahimiza washirikiane pia kuanzisha msingi mwingine wa madarasa mawili na yeye atawaunga mkono katika kupaua madarasa hayo kwa kuwa amejitoa kwa ajili yao na atahakikisha anawaunga mkono kwa kila juhudi ya maendeleo wanayoifanya na kusisitiza kuwa katika mambo ya upotoshaji hatokuwa pamoja nao.


“Dhamira yangu ni kuona Singida Mashariki inakuwa mpya na yenye maendeleo,mkurugenzi wa halmashauri kupitia idara ya ujenzi na afisa elimu niwaombe macho yenu yawe hapa, elekezeni namna ya kufanya kwa ajili ya matundu ya vyoo na nyumba za walimu ili tuweke mazingira mazuri tuombe usajili haraka kwa shule ya Simbikwa ili mwakani ianze kazi,”aliongeza mbunge huyo.

Mhe Mtaturu anaendelea na ziara yake jimboni humo kabla ya kuhudhuria vikao vya kamati ya bunge vinavyotarajiwa kuanza mapema wiki ijayo.