- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MHANDISI NYAMHANGA ATAKA HALMASHAURI ZIJIBU NA KUFANYIA KAZI MAPENDEKEZO YA CAG.
DODOMA: Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa hoja zote zilizoibuliwa kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinajibiwa na kufanyiwa kazi mapendekezo ya wakaguzi kwa kuanzia na wakaguzi wa ndani.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha upokeaji na uhakiki wa taarifa za majibu na mipango kazi ya utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya CAG kwa hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2017/18 leo katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo jijini Dodoma, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa ni muhimu hoja zote zikafanyiwa kazi haraka na kwa ufasaha ili kunusuru upotevu wa fedha, kuboresha utendaji na kuimarisha utawala bora, jambo ambalo ndio msingi wa ukaguzi.
Amesema kuwa ni vema kila Mtumishi afanye kazi kwa kuzingatia sheria, Kanuni, Miongozo, Taratibu na kuwajibika bila kuoneana haya.
“Tukifanya hivyo, hoja zisizo za lazima zitaondoka na hata wakaguzi hawatatumia muda mwingi katika kufuatilia mambo ya msingi zaidi katika kuboresha utendaji,” amesema.
Kauli ya Katibu Mkuu Nyamhanga inafuatia kukamilika kwa zoezi la kujibu hoja za CAG lililofanywa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Waweka hazina na Wakaguzi wa Ndani kutoka Halmashauri zote 185, zoezi lililoanza tarehe 19 na kukamilika tarehe 26 machi, 2019.
Mhandisi Nyamhanga ameongeza kuwa katika kujibu hoja za CAG na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo ya CAG ya Hesabu za mwaka 2016/17 imeonekana kuwa kufikia mwezi januari 2019, jumla ya hoja asilimia arobaini na saba (47%) zilifungwa wakati asilimia 53% zilikuwa bado hazijajibiwa.
Katibu Mkuu amesema kuwa zoezi hilo liliendelea katika ukaguzi wa Hesabu za Mwaka 2017/2018 ambapo hali halisi ya utekelezaji wa maagizo ya CAG zitaonekana baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa bungeni mwaka 2019.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji wa fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa Bi Miriam Mmbaga amesema kuwa kikao hicho kimefanyika kuanzia tarehe 19-26 Machi, 2019 ambapo kimewahusisha Wakurugenzi, Waweka Hazina na Wakaguzi wa Ndani kutoka Mikoa 26 na Halmashauri zote 185 nchini.
Amesema lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwawezesha Watendaji hao kujibu hoja za CAG, kuongeza uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi ili hoja hizo zisijitokeze tena katika halmashauri zao.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba akiongea kwa niaba ya Wakurugenzi wa Halmashauri amesema kuwa halmashauri zimekuwa zikikabiliana na changamoto mbalimbali katika kujibu hoja za ukaguzi kwani hoja nyingine hasa zile za kisera zilipaswa kujibiwa na Wizara husika badala ya ilivyo sasa kujibiwa na halmashauri.
Pia amewaasa wakurugenzi wenzake wa halmashauri kuwapa ushirikiano wakaguzi wa ndani wa halmashauri zao pindi wanapohitaji magari kwa ajili ya kwenda kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri zao.