- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MH MTATURU AJA NA MRADI WA KOPA NG'OMBE LIPA NG'OMBE.
DODOMA: Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameahidi kuanzisha mradi wa kukopesha wananchi ng`ombe wa maziwa ambao watasambazwa katika tarafa mbili ziliopo katika jimbo hilo.
Ahadi hiyo ni miongoni mwa vipaumbele vyake vitano alivyovitaja katika kuwatumikia wananchi.
Akizungumza na Mwakilishi Online,Mtaturu ambaye mbali na kuwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Ikungi alikuwa pia katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Mwanza ametaja tarafa hizo kuwa ni Mung`aa na ikungi.
“Nimekuja na mradi kwenye ngazi ya kaya wa kopa ng`ombe lipa ng`ombe,katika kutekeleza mradi huu nitatafuta mitamba 20 ambayo nitaigawa kwa tarafa hizo mbili,”alisema Mtaturu.
Amewataka wananchi kujiandaa kupokea ng`ombe hao kwa kujenga mabanda na kuwatunza kwa kutumia gharama zao hadi watakapozaa.
“Kwa mkamuo mmoja ng’ombe anaweza kutoa maziwa wastani wa lita 10 kwa siku ambayo watauza kwa wastani wa sh 1000 kwa kila lita,hii maana yake itawawezesha kujikimu katika malazi,chakula na tiba,”aliongeza Mtaturu.
Amesema kuna baadhi ya wananchi mtoto akifika umri wa kwenda shule anashindwa kupelekwa kwa kutokuwa na sare hivyo ni lazima kubuni miradi mbalimbali ili iwasaidie kiuchumi ikiwemo kuhamasisha kilimo cha kisasa badala ya kile cha mazoea.
Vipaumbele vingine alivyovitaja ambavyo atahakikisha anavitekeleza ndani ya kipindi kifupi cha ubunge wake kilichobakia ni elimu ambapo amesema atahamasisha jamii kuunga mkono elimu bila ya malipo pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia.
Aidha atashirikiana na serikali katika kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa huduma za afya,huduma za maji na kuhamasisha wananchi kujiletea maendeleo.
Mtaturu alishinda kiti hicho Julai 11 mwaka huu ambapo alipita bila kupingwa baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Tundu Lissu kuvuliwa ubunge kwa kushindwa kujaza fomu za tamko la mali na madeni na kutohudhuria vikao vya bunge bila kutoa taarifa.