Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 10:23 am

NEWS: MGOMBEA ACT WAZALENDO ASEMA ATAENDELEA NA KAMPENI

Moshi. Mgombea pekee wa nafasi ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karikacha Moshi Manispaa mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Pamphil Shayo, amesema ataendelea na kampeni kama kawaida licha ya chama chake kutangaza kujitoa.

Msimamo huo ameutoa hii leo Jumapili Novemba 17,2019, mara baada ya kufanyiwa mahujiano na gazeti la Mwananchi.

Mgombea huyo amesema alikuwa azindue kampeni zake leo eneo la Rau madukani, lakini Chama cha Mapinduzi (CCM), kikampiku na kuzindua kampeni zake eneo hilo hilo alilokuwa amechagua.

"Mimi sikujitoa kwa sababu wale waliojitoa ni chama na taarifa za kuandika barua za kujitoa zilinifikia jana na muda wa mwisho wa kuwasilisha ulikuwa jana hiyo hiyo saa 10 (alasiri) nikashindwa," amedai "Sikuweza tena kuandika barua.

Nimeshaingia kwenye mchakato mrefu nikajikuta niko kwenye mchakato.

Ni lazima niendelee kwa sababu nitakwepaje? amehoji "Mimi kuwepo kwenye uchaguzi haimaanishi nimekisaliti chama changu bali hao (waliomtaka aandike barua) wamenifanya hivyo lakini mimi nitapambana nao tu hadi mwisho", Alipoulizwa atazindua lini kampeni zake, mgombea huyo amesema atazindua tu kwa staili tofauti na walivyofanya CCM kwa vile wao (CCM) walitumia ubabe kuchukua eneo na siku ambayo alipanga kuzindua.

CCM wilaya ya kichama cha Moshi mjini, leo kilizindua kampeni zake na kumtaka Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kwenda Moshi kumfanyia kampeni mgombea wake huyo ambaye ni pekee wa upinzani.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho leo Jumapili katika mtaa wa Karikacha kata ya Rau, Katibu wa Itikadi na Uenezi Moshi mjini, CCM Mohamed Mushi amesema kati ya mitaa 60, mitaa 59 wagombea wao walishapita bila kupingwa.

"Hapa Karikacha Zitto ana mgombea wake anagombea na ndio tunachuana naye hapa. Sasa Zitto asipotoshe umma kuwa wamejitoa, hapa anaye mgombea aje amsaidie kwa sababu hatatuweza" amesema Mushi katika mkutano huo.

Katibu huyo amesema mgombea huyo wa ACT- Wazalendo hatafua dafu na wanamtaka Zitto aende katika mtaa huo ili amsaidie mgombea wake kwani anaendelea kugombea na ndio pekee wanashindana naye baada ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa katika mitaa 59 kati ya 60.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa Madiwani wa CCM katika baraza la Manispaa ya Moshi, Priscus Tarimo, aliwatambulisha wenyeviti wa Serikali za Mtaa 59 ambao walipita bila kupingwa akisema sasa CCM ndio kina nguvu ya uamuzi wa kuwaletea wananchi maendeleo.

Vyama saba vya upinzani nchini kikiwamo ACT-Wazalendo vimeweka msimamo wa pamoja wa kususia uchaguzi huo na kilikuwa kimeagiza wagombea wake wote nchini kujitoa, wakilalanikia kukiukwa kwa kanuni na taratibu wa uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24,2019.