- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MEYA WA JIJI LA ARUSHANA WENZAKE 9 WAACHIWA HURU
ARUSHA: BAADA ya kusota rumande kwa siku tatu, hatimaye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro na wenzake tisa wakiwemo madiwani na viongozi wa dini waliokuwa wamekamatwa kutokana na kufanya mkusanyiko usio halali, wameachiwa huru jana.
Waliachiwa jana saa 12:30 asubuhi baada ya kudhaminiwa, huku kesho wakitakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa. Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembu, watuhumiwa hao wameachiwa baada ya kupata wadhamini.
Meya huyo na wenzake walikamatwa wakiwa katika Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha walikokwenda kutoa rambirambi kutokana na tukio la ajali ya basi la shule hiyo iliyopoteza maisha ya watu 35, wakiwamo wanafunzi 32, wawili wawili na dereva wa basi hilo.
Akizungumza baada ya kuachiwa, Lazaro alisema pamoja na kuswekwa rumande, dhamira yake ya kupeleka fedha zote za rambirambi kwa wafiwa badala ya kuzipeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, iko pale pale.
Akisimulia kukamatwa kwake katika viwanja vya shule hiyo, alisema aliongozana na viongozi wa dini kutoka Kanisa Katoliki Parokia ya Paloti, mashehe wawili ambao ni viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Kata ya Olasiti na Mwinjilisti wa Kanisa la Kilutheri la Tanzania (KKKT) Kata ya Olasiti.
Wengine ni madiwani wawili ambao ni Credo Kifukwe wa Kata ya Murriet, Alex Marti wa Kata ya Olasiti na wajumbe wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Kanda ya Kaskazini. Alifuatana pia na wanahabari ambao pia walikamatwa, lakini wakaachiwa baadaye.
Alisema wakiwa shuleni hapo na huku viongozi hao wakianza kwa sala, ghafla Polisi walikuja na kuwaeleza wapo chini ya ulinzi. Alisema walipandishwa kwenye magari ya polisi na walipofika polisi, viongozi wa dini na wanahabari waliambiwa wakae pembeni, kisha yeye, madiwani na viongozi wa umoja huo waliandikisha maelezo na kuswekwa mahabusu.
Alisisitiza kuwa, hajui ni kwa sababu gani waliwekwa selo. Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alielezea kusikitishwa na tukio hilo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amekuwa akiwasisitiza wanasiasa kuacha kuligeuza tukio la ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent kuwa mtaji wa kisiasa.
Aidha, amesema hakuna fedha yoyote iliyotafunwa na kuongeza kuwa, serikali ya mkoa wa Arusha iko katika harakati za kuwatumia fedha wazazi na timu ya wataalamu walioongozana na wanafunzi watatu walionusurika katika ajali hiyo ambao kwa sasa wamepelekwa nchini Marekani kwa matibabu zaidi kama fedha za kujikimu.
Habari leo