Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 6:48 pm

NEWS: MCHEZAJI WATANZANIA ADI YUSSUF AREJESHWA KWENYE CLUB YAKE

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Abdillahie ‘Adi’ Yussuf amerejeshwa kwa mkopo kwenye klabu yake, Solihull Moors FC ya Daraja la Tano, kutoka Blackpool FC ya Daraja la Tatu nchini England.

Taarifa ya Blackpool FC imesema kwamba Adi Yussuf aliyesaini mkataba wa miaka miwili Mei mwaka huu baada ya kumaliza mkataba na Solihull Moors amerejeshwa klabu hiyo kwa mkopo wa muda mfupi hadi Januari 5, mwakani.

Bado haijajulikana sababu za Yussuf mzaliwa wa kisiwani Zanzibar, mwenye umri wa miaka 27 kutolewa kwa mkopo miezi mine tu tangu ajiunge na Blackpool yenye maskani yake Lancashire.

Yussuf alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka huu nchini Misri.
Alitua Blackpool baada ya kufunga mabao 21 katika mashindano yote Solihull Moors, yakiwemo mawili dhidi ya Seasiders kwenye mchezo wa marudiano wa Raundi ya Pili ya Kombe la FA na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye National League.

Mchezaji huyo wa zamani wa akademi ya Leicester City, rekodi yake nzuri zaidi ya msimu ni kufunga mabao 29 katika mechi 39 akiwa na Oxford City msimu wa 2014- 2015 baada ya awali kuchezea Burton Albion, Mansfield Town na Crawley Town.

#Binzubeiry