Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 8:43 am

NEWS: MCHEKESHAJI MASANJA AJISALIMISHA KWA DC KATAMBI DODOMA

Mchekeshaji maarufu nchini Tanzania Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja mkandamizaji amewasili leo Aprili 4, 2020 Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuitikia wito uliotolewa jana na DC wa wilaya hiyo Bw. Patrobas Katambi, akimtaka Mchekeshaji huyo kujisalimisha ofisi ya DC au Polisi Dododoma kwa mahojiano.

DC Katambi ametoa agizo hilo kwa Masanja jana baada ya kusambaa kwa video ya kipindi chake ambacho hurushwa na Kituo cha Televisheni cha Kimataifa cha DW, ambapo alikua akihoji wananchi wa Dodoma kuhusiana na virusi vya Covid19 ambavyo huchangia maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Akizungumza na wandishi wa habari, DC Katambi amesema mchekeshaji huyo alikua akiufanyia mzaha ugonjwa wa Corona ilihali serikali inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo.

" Licha ya viongozi wetu wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Magufuli kuwataka wananchi kufuata ushauri wa watalaamu katika kujikinga na ugonjwa huu, kumetokea utani wa kuufanyia mzaha ugonjwa huu akitaka kuthibitisha kuwa wananchi wetu hawana uelewa wowote wa Corona.

Sasa kwa mzaha huo tunataka kujua malengo yake na kwanini amefanya hivyo Dodoma wakati hata Kituo chake cha DW nchini Ujerumani wameuchukulia serious, sasa kwanini hawajafanya utani huo sehemu nyingine zaidi ya Tanzania na haswa Dodoma. Sasa nimtake afike Ofisi ya Mkuu wa Wilaya au Vituo vyetu vya Polisi ndani ya siku tatu," Amesema DC Katambi.