- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MBUNGE WA KIBITI : ''NAMUACHIA MUNGU''
PWANI : MATUKIO ya kihalifu na mauaji yanayofanywa na watu wasiofahamika, yameendelea kutokea wilayani Kibiti baada ya viongozi wawili wa Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, huku Mbunge wa Jimbo la Kibiti akisema anamuchia Mwenyezi Mungu kutokana na mauaji hayo.
Viongozi waliouawa usiku wa kuamkia jana ni Hamis Mkima ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi na Mtendaji wa kijiji hicho, Shamte Rashid. Alipoulizwa kuhusu mauaji yanayoendelea Kibiti, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando (CCM), hakuwa tayari kuzungumzia kwa kina matukio ya kihalifu na mauaji yanayotokea zaidi ya kusema, “Sina cha kuzungumza, namuachia Mungu.
Tangu kuanza kwa mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo, zaidi ya watu 35 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwamo polisi 13. Akizungumza na gazeti hili jana, Mtendaji wa Kata ya Mchukwi, Ami Ali aliwataja waliouawa ni Mkima ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi na Mtendaji wake, Rashid.
Ali alisema siku hiyo ya tukio, watu wenye silaha walienda nyumbani kwa mwenyekiti wakamteka na wakamlazimisha awapeleke kwa viongozi wengine wa kijiji hicho. “Walipomteka, inasemekana mwenyekiti alijaribu kuwatoroka ndipo walimpompiga risasi ya mguu na kuondoka naye hadi kwa Nuru Njukute ambaye ni mmoja viongozi wa kitongoji kimojawapo kijiji hapo,” alieleza mtendaji huyo wa kata.
Alisema hata hivyo hawakumkuta mtendaji huyo, ndipo walipoondoka na mwenyekiti huyo hadi kwa mtendaji wa kijiji na kuingia ndani na kuwatoa nje yeye na familia yake. Alisema walivyomtoa nje na familia yake, walimchukua na kuzunguka naye nyuma ya nyumba na huko wakampiga risasi tatu na kumuua hapo hapo.
“Walivyomaliza kufanya mauaji hayo walichoma nyumba yake na wakaondoka eneo hilo na mateka wao,” alisema mtendaji huyo. Alisema mateka huyo aliwapeleka kwa kiongozi wa Kitongoji wa Londo, Michael Nicholaus ambaye alivyosikia hodi alipitia mlango mwingine akijaribu kutoroka, lakini wakampiga risasi ya kichwa ikatokea kwenye jicho.
“Hata hivyo, bahati nzuri kiongozi huyo wa kitongoji hakufariki, alijeruhiwa tu, na sasa amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alieleza na kuongeza kuwa walipomaliza kufanya unyama huo, ndipo walimpogeukia mateka wao na wakampiga risasi na kumuua hapo hapo.
Alisema polisi walifika eneo hilo jana asubuhi wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro. “Sirro amefika hapa na amewapa pole wananchi na amegeuza jioni hii,” alieleza mtendaji huyo.
“Kwa kweli mazingira yetu ni ya hatari, wananchi wanahitaji huduma, lakini na sisi wenyewe hali ndio kwani tukio hili la kutisha katika kata yangu,” aliongeza mtendaji huyo. Kuhusu viongozi waliouawa, Ali alisema wamewazika wote kwa pamoja jana jioni katika eneo moja.
Alisema kitendo cha viongozi wawili kuuawa katika eneo lake na mmoja kujeruhiwa linamfanya hata yeye kuwa na wasiwasi na maisha yake. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alikiri kutokea mauaji hayo na na kusema wanaendelea kufuatilia ili kuwabaini wahusika wa matukio hayo.
Katika hatua nyingine, Chama cha ACT Wazalendo kimeungana na wananchi wote na wapenda amani nchini kulaani mauaji hayo na kuongeza kuwa wanaona mauaji hayo kama tishio na jaribio juu ya uhuru na usalama wa Taifa.
Taarifa iliyotumwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa ACT Wazalendo, Mohammed Babu, ilimnukuu kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe akisema: “Tunahitaji kushikamana kama nchi kwenye suala la Mkiru (Mkuranga, Kibiti na Rufiji).
Mauaji yanayoendelea huko hayapaswi kupewa nafasi kuendelea. Taifa lizungumze lugha moja kukabiliana na hali hii. “Ninarejea wito niliotoa siku zilizopita kuwa ninatarajia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama itakwenda eneo la Mkiru kuzungumza na wananchi wa kule ili kupata maarifa ya kuishauri na kuisimamia serikali kudhibiti mambo na kuimarisha usalama.”
Alisema mambo hayo yanatuunganisha taifa bila kujali itikadi, dini, hali ya kiuchumi wala rangi. “Hatuamini kwa namna yoyote kuwa wauaji hao ni watu wenye nia njema wala ajenda ambayo njia pekee ya kuifikia ni kupitia mauaji ya Watanzania wenzao.
Hawa ni wahalifu na wanaostahili nguvu ya umoja wetu dhidi ya udhalimu wao,” alieleza. Imeandikwa na John Gagarini (Kibaha) na Shadrack Sagati (Dar).
source; habari leo