Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 9:44 am

NEWS: MBUNGE JAGUAR AKAMTWA NA VYOMBO VYA USALAMA KUTOKANA KAULI YA KIBAGUZI

Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles Njagua maarufu Jaguar Nchini Kenya amekamatwa leo nje ya jengo la Bunge la nchi hiyo, kutokana na kauli yake aliyoitoa Juzi akiwataka Wafanyabiashara kutoka nchi za Tanzania na Uganda kuondoka mara moja nchini humo ndani ya saa 24 vinginevyo watapigwa na wananchi.

Jaguar amekamatwa kwenye mwendo wa saa 6:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki na askari jeshi la polisi waliokuwa wamevaa kiraia na kisha kupandishwa kwenye gari la polisi.

siku mbili zilizopita Jaguar ambaye ni mwanamziki wa kibao cha 'Kigeugeu ' alitembelea kwenye moja ya sehemu ya jimbo lake la starehe katika soko moja la jijini Nairobi na kutoa kauli kali na yakibaguzi, Kauli ambayo ilisababisha taharuki ya kidiplomasia baina ya nchi za Afrika Mashariki. “Kama utatembelea masoko, Waganda na Watanzania dio waliochukua biashara yote. Sasa tunasema imetosha. Kama wataona muda wa saa 24 wa kuondoka haraka nchini hautoshi, tutawaondoa kwa nguvu na tutawapiga na hatutamuogopa mtu,” alisema Njaguar.

Jana, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliliambia Bunge kuwa Serikali imezungumza na Balozi wa Kenya nchini pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya kuhusu kauli hiyo. Alisema kuwa Serikali ya Kenya imeeleza kuwa kauli ya Njagua sio msimamo wa Serikali na kwamba ni kauli yake binafsi.

Hata hivyo, jana Njagua aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter akieleza kuwa hakumaanisha Watanzania na Waganda, jambo ambalo lilisababisha watu wengi wamshambulie.

“Kauli zangu zilikuwa zinaunga mkono maelekezo ya Waziri Matiang’i yakimaanisha Wachina waliongia kwenye masoko yetu kufanya biashara, hali ambayo haivumiliki kwa wananchi. Siko kinyume na muungano wa jumuiya [ya Afrika Mashariki] unaohuisha biashara kati ya jumuiya hiyo,” alitweet.

Juni 12, 2019, Waziri Matiang’i aliagiza kuondolewa mara moja kwenye masoko wafanyabiahara wa kigeni [hasa Bara Asia] ambao wanafanya biashara za kawaida kwenye masoko ya Kenya.

Hatua hiyo ya Matiang’i ilikuwa ikijibu kilio cha wafanyabiashara wa Kenya ambao walidai kuwa Wachina wameingia kwenye soko la Nairobi la Gikomba kufanya biashara kinyume cha taratibu ambazo zinawataka kuwa wawekezaji kwa kiwango fulani cha mitaji.