Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:36 pm

NEWS: MBUNGE CUF AWATUHUMU POLISI KUWAPIGA WAPINZANI

Dodoma. Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma amelituhumu Jeshi la Polisi kuwapiga wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania.

Baada ya kutoa tuhuma hizo bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Februari 4, 2020, Serikali ya Tanzania imesema tuhuma hizo ni nzito na kumtaka atoe ushahidi wa kutosha.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo, Nachuma amesema katika maeneo mbalimbali nchini hasa Mtwara, wananchi ambao ni wanachama wa upinzani wamekuwa wakiamshwa majumbani usiku na kuanza kupigwa bila sababu za msingi.

"Polisi ni chombo muhimu katika kulinda haki za raia na mali zao, lakini wanaposhindwa kutimiza wajibu wao inakuwa ni tatizo na kero kwa Watanzania," amesema Nachuma.

Amesema kitendo hicho kinakiuka kanuni na taratibu katika sheria za vyama vingi nchini Tanzania na kuiomba Serikali kutoa tamko la kuzuia vitendo hivyo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amesema tuhuma hizo ni nzito na kumtaka mbunge huyo ambaye ni makamu mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara kupeleka vielelezo serikalini.

Masauni amesema ataongozana na mbunge huyo kupita maeneo yote ambayo yanalalamikiwa na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo.