Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:51 am

NEWS: MBOWE AMBURUZA DC WA HAI MAHAKAMANI

Kilimanjaro: Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe leo amefungua kesi dhidi ya mkuu wa wilaya wa HAI Dr. Gelasius Byakanwa akidai fidia ya Tsh 549 million kwa kuharibu miundombinu ya shamba, Mbowe kupitia Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Limited (KVL), inayomilikiwa na yeye mwenyewe Mbowe Kiini cha kesi hiyo ni hatua ya mkuu huyo wa wilaya akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama, kuharibu miundombinu ya umwagiliaji ya shamba (Green House) la kampuni hiyo Juni 19.


Katika kesi hiyo ya ardhi namba 20/2017 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Moshi, Mbowe ambaye ni mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni hiyo, amemshtaki mkuu huyo wa wilaya kama mtu binafsi Hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani na Wakili Meirad D'Souza wa jijini Arusha, Mbowe alilalamikia kitendo cha Dk. Byakanwa kuingia kwa jinai katika shamba hilo na kufanya uharibifu huo.


Mbowe katika kesi hiyo ya msingi anasema Dk. Byakanwa hakuwa na mamlaka ya kisheria kufanya alichokifanya na kuiomba mahakama itoe zuio la kudumu kwa mashtaka kutoingilia shughuli za KVL.
Pia, anaiomba mahakama imuamuru mshtakiwa kulipa fidia maalumu (special damages) ya Sh 549. 3 milioni inayotokana na uharibifu wa mali, usumbufu na hasara ambayo KVL imepata.
Kampuni hiyo inaiomba mahakama imuamuru mshtakiwa kulipa riba ya asilimia 25 ya fedha hizo, na aamriwe kulipa gharama za kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wa jimbo hilo na nchi nzima.

Mbali na kesi ya msingi, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai (Chadema), amewasilisha maombi namba 51/2017 akiambatanisha kiapo cha kutaka kesi hiyo isikilizwe chini ya hati ya dharura.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo alithibitisha kufunguliwa kwa kesi hizo na kwamba maombi ya usikilizwaji wa dharura yamepangwa kufanyika Jumatatu ijayo.
Kwa mujibu wa Mpepo, Jaji Mfawidhi pia ameagiza mdaiwa (Byakanwa) apelekewe nyaraka za kesi hiyo na awe amewasilisha majibu yake kabla ya usikilizwaji wa maombi Julai 17.


Mbowe alipotafutwa mwishoni mwa wiki iliyopita kuzungumzia kesi hiyo, alithibitisha kuifungua lakini akashauri atafutwe wakili wake, huku Dk. Byakanwa akisema amepata notisi ya kesi hiyo.