Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 4:42 pm

NEWS: MBOWE ALAANI VIKALI KAULI YA MAKONDA MSIBANI KWA MENGI

Kilimanjaro: Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe amelaani vikali vitendo na Kauli za ubaguzi wa kikabila,Rangi, Dini na kisiasa huku akisema ni vyema kuchunga kauli zinazotolewa kama zitaweza kujenga, lakini siyo kuwabaguwa watu katika makundi.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni amezungumza maneno hayo leo, Alhamisi, Mei 9, 2019 wakati akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kumuombea aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi inayofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Moshi Mjini.

"Naomba niseme jambo moja ambalo limetukwaza wengi na kwa sababu sina tabia ya unafiki nitasema ‘straight’ ni nchi moja ambayo tunastahili kupendana, kujengana, kuheshimiana na kumuona kila mmoja wetu ni sehemu ya nchi,” amesema.


“Tusikubali matendo na kauli za kibaguzi zikatubagua katika nchi yetu, tutapoteza Utanzania wetu sifa ambayo tumejivunia kwa miaka mingi.”

Kauli hii ya Mbowe iliwafanya waombolezaji wa ndani na nje kushangilia kwa kupiga makofi.


“Anapotokea kiongozi mwenye mamlaka akatoa kauli ya kubeza kabila fulani, tukaanza kubaguana kwa makabila au kwa dini siyo mambo mema, lazima wote tuungane kila mmoja kwa nafasi yake tukakemea jambo hili,” amesema Mbowe.


“Tusianze kubaguana kwa itikadi, tusibaguane kwa imani, tusibaguane kwa makabila yetu, tupendane na kutambuana kama Watanzania, kauli za kuambiana kuwa kuna kabila fulani haliwezi kuwatetea walemavu si za kweli ni za kibaguzi na lazima tuzikemee.”

Mbunge huyo wa Hai pia akasema, “naomba wote walioguswa na kauli zile tutoe msamaha kumuenzi mzee wetu Mengi, tusamehe, lakini tusiwe wanafiki tujifunze kusema ukweli na kweli itawaweka huru.”

Amesema katika mazingira ya kibinadamu kuna mambo mawili yanayojenga kiburi ambayo ni mamlaka yasiyotumiwa vizuri na fedha zisizotumika kwa unyenyekevu.

Kauli hiyo ya Mbowe ni majibu kwa kauli aliyoitoa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda aliyoitoa hivi karibu wakati wa kuaga mwili wa Dkt Mengi Katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es salaam akisema kuwa hakuna mchaga anayeweza kusaidia walemavu kama mengi.

“Mzee Mengi hakuwa kiongozi wa kisiasa, lakini alikuwa mnyenyekevu, utajiri wake haukumtia kiburi, bali ulimuongezea unyenyekevu na msaada kwa wengi ambao aliwajua na ambao hakuwajua.”

Mbowe amesema, “hivyo kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani. Niombe sana Watanzania wenzangu kama tulivyokuwa kwa pamoja na kukaa pamoja kwa dini zote, kabila zote, vyama vyote niombe basi tuuendeleze unyenyekevu kwa siku zote na siyo tuuonyeshe tunapokuwa kwenye matatizo.”