Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 1:55 pm

NEWS: MBATIA BADO ALILIA TUME HURU YA UCHAGUZI

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, nchini Tanzania James Mbatia amesema msimamo wa kama chama tangu mwaka 1991 ni kuwa na Katiba mpya ambayo ndani yake kuna Tume huru ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia

Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne, Machi 10 wakati akifanyiwa mahojiano na MCL Digital, Mbatia amesema suala la Tume huru ya uchaguzi lilizungumziwa na Tume ya Jaji (Francis), Tume ya Jaji Robert Kisanga na Tume ya Jaji, Joseph Warioba. “Sisi NCCR Mageuzi, tangu kuasisiwa kwetu mwaka 1991 ndiyo tulianzisha National Committee for Constitution Reform.

Tunazungumzia Katiba mpya yenye kufuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na Tume ya uchaguzi ni mtoto wa Katiba mpya,” amesema Mbatia.

“Sisi mpaka leo hii, msimamo wetu bado ni wa kuwa na Katiba mpya inayotokana na umma. Tuwe na makubaliano ya kimataifa, namna gani tuendeshe chaguzi zetu tukiwa na Tume inayokubalika na pande zote.”

Aidha Mbatia amezungumzia suala la Mshauri Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad na Prof. Ibrahimu Lipumba kuitwa Ikulu, huku akisema kuwa swala hilo hakulifahamu kabla mpaka alipoliona kwenye Vyombo vya Habari

Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia, (TCD) amesema awali walimwandikia barua Rais Magufuli wakimwomba akutane na vyama vya siasa, asasi za kiraia na madhehebu ya dini.

“Ombi letu tangu mwanzoni mwa 2018 tulihitaji meza ya mazungumzo ya pamoja. Hata juzi sikujua kama Maalim Seif ameitwa, wala sikujua kama Lipumba ameitwa sikujua kabisa. Nilikuja kusoma kwenye vyombo vya habari lakini sikujua wamezungumza nini.”

“Tangu tulipokutana kwenye summit ya TCD mwaka 2017 kule St Gasper Dodoma, tukaja kukutana steering committee (kamati tendaji), ombi letu la awali ni kukutana na uongozi wote, ndiyo msimamo wetu na ndicho tulichoomba,” amesema

Machi 3, 2020 Rais Magufuli alikutana kwa nyakati tofauti na Maalim Seif, Lipumba na Mbatia Ikulu jijini Dar es Salaam na baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao wa upinzani walieleza walichozungumza na rais ikiwa ni pamoja na suala la uchaguzi huru na haki.