Baraza la Wawakilishi Marekani limepitisha mswada mpya wa kichocheo cha uchumi wa dola bilioni 483 wakati kiwango cha ukosefu wa ajira kutokana virusi vya corona kikipanda na makampuni yakihitaji msaada zaidi. Mswada huo tayari ulikuwa umeidhinishwa na Baraza la Seneti, na Rais Donald Trump ameashiria kwamba atausaini haraka iwezekanavyo kuwa sheria. Mpango huo unaongeza kwa ule wa trilioni 2.2 ulioidhinishwa mwishoni mwa Machi.
Karibu watu 50,000 wamefariki dunia Marekani kutokana na virusi vya corona, huku idadi ya walioambukizwa ikifikia 866,646. Spika wa bunge Nancy Pelosi alisema mpango huo ni muhimu kwa kuzilinda familia za Marekani na kuhakikisha kuwa kampuni ndogo ndogo zina rasilimali zinazohitaji.