Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:58 am

NEWS: MANJI ASOMEWA UHUJUMU UCHUMI KITANDANI MUHIMBILI

DAR ES SALAAM: MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji (41) na wenzake watatu, wamesomewa mashitaka ya uhujumu uchumi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam jana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhamia hospitalini hapo.

Mahakama hiyo imefanya uamuzi wa kuhamia katika hospitali hiyo kutokana na Manji kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Manji alikuwa amelazwa katika wodi namba moja na alisomewa mashitaka hayo huku akiwa kitandani.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43) mkazi wa Chanika ambao walisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tulumanywa Majigo alidai jana kwamba Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A wilayani Temeke Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni 192.5.

Majigo alidai Julai mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh milioni 44.

Katika mashitaka ya tatu, inadaiwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A, washitakiwa walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa “Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ” bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.

Pia inadaiwa tarehe hiyohiyo maeneo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma” bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama.