Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 5:00 pm

NEWS: MAKAMU RAIS AWAONYA VIKALI WANACCM WANAOTAFUTA UBUNGE MAPEMA

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya vikali wanachama wenzake na makada wa chama cha Mapinduzi (CCM ) walioanza kujipitisha pitisha katika majimbo kuweka mazingira ya kupitishwa kuwania nafasi ya Ubunge kwa mwaka 2020.

Bi Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2020 katika maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema chama hicho kina taratibu zake katika kusimamia uchaguzi na kwamba muda ukifika wote wataruhusiwa kutangaza nia na kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao.

"Kuna fununu kwamba baadhi ya watu wameanza kujipitisha pitisha huko majimboni. Ninawaomba mfuate kanuni na taratibu za chama.” " Kama wewe ni mchezaji, subiri filimbi ipigwe ndipo uanze kucheza, sio unaanza kucheza peke yako, filimbi ikipigwa mpira unakukuta uko golini, unatia,”amesema Samia.

Amewataka wanachama wa CCM kupendana na kwenda kwenye uchaguzi mkuu wakiwa wamoja. Amesema kufarakana miongoni mwao ni chanzo cha kuwapa ushindi wapinzani.

“Msitupunguzie mtaji mapema hivyo kwa sababu mkisimamisha, mkifukuza watu sasa hivi, kila mnayemfukuza ana ndugu, jamaa na marafiki, watamuunga mkono kwenye nongwa yake aliyo nayo, kwa nini mtengeneze nongwa sasa hivi?” amesema Bi Samia

Amesisitiza kwamba mtu anayefaa kugombea apewe nafasi hiyo badala ya kuondolewa sifa au kuvuliwa uanachama ili mradi asipate nafasi kwa sababu tayari viongozi wana watu wao. "Mtu anafaa kugombea lakini anaandikiwa sifa mbovu, kisha anaenguliwa.Mwenendo huu hautupeleki kuzuri, tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu tushikamane ili twende pamoja, tushinde pamoja," amesema Samia.