- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAJI YAMLIZA MBUNGE WA MORO
Dodoma: Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood (CCM), ameiomba serikali kuharakisha utekelezaji mradi wa kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Morogoro ili kuondoa kero ya maji kwa wakazi wa eneo hilo.
Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/18, Abood amesema manispaa hiyo inakabiliwa na kero ya maji kwa muda mrefu.
“Naishukuru serikali na Rais John Magufuli kwa kutupatia mradi wa maji. Naomba mradi huu tuliopewa na Wafaransa uharakishwe ili kuondoa kero ya maji hasa kwa wakazi wa Morogoro ambao wameongezeka,” amesema.
Amesema kuna eneo la uwekezaji ndani ya manispaa hiyo ambalo watu wanataka kuwekeza kwenye viwanda lakini halina maji.
“Wawekezaji wakija, kitu cha kwanza wanauliza maji. Kwa hiyo, naomba wizara iharakishe kazi hii ya mradi huu wa maji ili tupate maji kwa wakati,” amesema.
Abood amesema Bwawa la Mindu lililopo katika manispaa hiyo limejaa, lakini bado miundombinu ya kusambaza maji maeneo mbalimbali ya Morogoro bado ni tatizo.
“Wananchi wa Mindu ambao wanalilinda bwawa, cha kushangaza maji hawana wala miundombinu. Wizara iliangalie ili kuondoa kero hiyo,” amesema.
Mbali na changamoto hiyo, mbunge huyo aliiomba wizara kusaidia kutatua mgogoro kuhusu miradi ya Benki ya Dunia (WB) ambayo wananchi walichangia lakini sasa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Morowasa) inataka kuichukua huku wananchi wao wakitaka waiendeshe wao wenyewe.
Mbunge huyo pia amesema kuna tatizo la ankra za maji ambapo wananchi wanalipishwa bila kutumia maji mwezi mzima.
Awali akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, alisema serikali imeanza kutekeleza mpango wa muda mfupi wa uchimbaji wa visima vitano kukabiliana na upungufu wa maji katika manispaa hiyo.
Alisema hadi Machi 2017, visima vitatu vilichimbwa na vilipata maji na viwili vilivyobaki vinatarajiwa kukamilika mwezi huu.
Katika mwaka wa fedha 2017/18, Mhandisi Lwenge alisema serikali imetenga Sh. milioni 500 kwa ajili ya kuendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika manispaa hiyo.
Kwa upande wa mpango wa muda mrefu, waziri huyo alisema serikali kwa kushirikiana na Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), itatekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji na unatarajiwa kuanza mwaka ujao wa fedha.