Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:43 am

NEWS: MAJAMBAZI WAWABAKA WAHUDUMU WOTE WA GESTI NA KUPORA PESA

MBEYA: Majambazi watatu, wamevamia nyumba ya kulala wageni ya Malema Lodge katika mtaa wa Sinde jijini Mbeya, kisha kufanya ubakaji kwa wahudumu na mlinzi na hatimaye kupora fedha.

Lodge hiyo inayomilikiwa na Diwani Viti Maalumu (CCM), Mary Malema,

Unyama huo waliufanya usiku wa kuamkia jana Januari 26 baada ya kuwapa ofa ya vinywaji na biskuti zinazodaiwa kuwa na dawa za kulevya na Kisha kuwabaka wote.

Shuhuda wa tukio hilo (jina linahifadhiwa), alisema watu watatu waliingia ndani ya baa hiyo wakiwa kama wateja na kuanza kutoa ofa za vinywaji na biskuti na kwamba yeye aliondoka baada ya muda kufika na kwamba alipata taarifa kuwa baada ya kula vitu hivyo, walilala wakiwa hoi.

Alisema baada ya kuzidiwa kutokana na kulewa, watu hao watatu walianza kuwabaka wanawake hao hata kufikia hatua kuwaingilia kinyume cha maumbile kisha kupora fedha ambazo thamani yake haijafahamika na kwamba asubuhi alipokuwa anapita, aliona msamaria mwema amewabeba na kuwapeleka hospitali akipitia polisi.

Waathirika wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya wakiwa hawajitambuhi wakipumulia mashine.

Malema ambaye pia ni diwani wa viti maalumu katika kata ya Manga, alisema wakati anapita aliona msamaria mwema anawabeba ndipo katika kuchunguza akabaini kuwa vijana wake waliingiliwa na watu hao.

Alisema alikwenda polisi akapewa barua kwa ajili ya matibabu. ‘’Watu hawa kuna uwezekano mkubwa wanafahamika.

Wamevamia gesti zenye baa maeneo mbalimbali na hawakamatwi. Polisi walipowaona vijana hawa wakiwa hoi wakasema wamepewa biskuti, wamejuaje?” alihoji na kusema: “Hadi muda huu (akizungumza na mwandishi wa habari hii), hakuna polisi aliyefika kuwaona wala kufuatilia tatizo hili, ’’alisema Malema. Alisema alipofika baa alikuta fedha zote zimechukuliwa na zikiwamo pia na za upande wa gesti na kwamba hajajua kiasi cha fedha kwa kuwa hawakufunga hesabu.

Aliliomba jeshi la polisi kufuatilia kwa kina suala hilo kwa kuwa vijana wake (majina yanahifadhiwa) wamelazwa hospitalini pamoja na mlinzi aliyemtaja kwa jina la Dickson. Raykiza Ntepa, ofisa Mtendaji kata ya Manga, licha ya kukiri kuwapo kwa taarifa hiyo, alisema wako kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya tarafa ya Eying, kujadili mambo kadhaa, likiwamo tukio hilo na kwamba watafuatilia ili kuwabaini wahusika.

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema hajapelekewa taarifa juu ya tukio hilo na mkuu wa polisi wilaya na kwamba atahitaji apate taarifa hizo ili kujua undani wake sambamba na kuweka mikakati ya watuhumiwa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.