Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 12:48 pm

NEWS: MAJALIWA: ''UWEKEZAJI WENU HAPA NCHINI UTAKUWA NA BARAKA''

DAR ES SALAAM: WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewahakikishia uwekezaji wenye tija wawekezaji watakaokuja nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu wa kisiasa na uchumi wenye kukua kwa kasi.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salam jana alipomuwakilisha Rais John Magufuli katika maadhimisho ya miaka 60 tangu Mtukufu Aga Khan alipochaguliwa kuwa Imamu Mkuu wa madhehebu ya Shia Ismailia duniani. Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbalimbali zinazofanywa na mtandao wa taasisi za Aga Khan zilizopo hapa nchini, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana nao.

Aliupongeza mtandao wa taasisi za Aga Khan kwa kumuunga mkono Dk Magufuli katika kutoa kipaumbele cha kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili waweze kujikwamua kiuchumi. “Nawahakikishia kwamba uwekezaji wenu hapa nchini utakuwa na baraka kwa sababu nchi imetulia kisiasa na uchumi wake unakua kwa kasi.

Nawaomba muendelee kuwaalika wanajumuia wa madhehebu ya Shia Ismailia popote walipo duniani waje kuwekeza nchini fursa bado zipo.” Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Madhehebu ya Shia Ismailia Tanzania, Amin Lakhani ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapa na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana nayo katika kuboresha sekta mbalimbali nchini.

Alisema mtandao wa maendeleo wa Aga Khan unatoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, kilimo na kunaendesha miradi katika mabara ya Afrika na Asia kwa kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi. Awali, Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema aliipongeza taasisi hiyo kwa mpango wake wa upanuzi wa hospitali na kuongeza vituo 35 vya afya kutoka 15 walivyonavyo.