Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 1:20 am

NEWS: MAJALIWA: '' TUACHE KUWATUMIA WATOTO WADOGO KAMA VIBARUA''

TABORA: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora, wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalumu.

“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema Majaliwa kwa mujibu wa taarifa ya ofisi yake kwa vyombo vya habari.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari. “Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao.

Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema. Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara yake ya siku nne moani Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30.

Pia aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao pia wana hatari ya kuhukumiwa kifungo cha miaka.

#Habarileo