Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:57 am

NEWS: MAJALIWA:' HATUZUII KUUZA MAZAO NJE'

DODOMA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amejibu hoja zinazosambazwa na wanasiasa wa kambi ya upinzani juu ya zuio la chakula nje ya nchi, akisema Serikali haizuii fursa ya wakulima kuuza mazao nje.

Bali, amesisitiza serikali inataka mazao hayo yatosheleze nchini na kama ni lazima, basi kwanza yasindikwe, yabanguliwe, yachakatwe kwa kuyakoboa ili kuyaongezea thamani. Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja ya wapinzani, walioitisha mkutano wa waandishi wa habari juzi na kuilaumu serikali.

Alhamisi wiki iliyopita, wakati Waziri Mkuu akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati aliyetaka kuruhusiwa kuuzwa mahindi nje ya nchi, alikataza kuuza mahindi nje ya nchi.

Alisema ni marufuku kuuza mahindi nje ya nchi; na kama ni muhimu lazima kibali kitoke kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi; na uuzwe unga uliosagwa na kamwe yasiuzwe mahindi.

Waziri Mkuu alitetea kauli hiyo ya serikali jana wakati akikagua banda la Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Kilimo cha Umwagijiaji Dakawa (UWAWAKUDA) kabla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM wa Jakaya Kikwete mjini hapa.

Alimpongeza na kumsifu mkulima Nassib Katoto kwa niaba ya wakulima wenzake wa Mpunga Dakawa mkoani Morogoro, kutokana na kulima kilimo cha umwagiliaji, lakini hasa kuvuna mpunga, kuukoboa na kuusindika ili kupata mchele na kuuweka katika mifuko na kuuza baada ya kuongeza thamani, badala ya mpunga.

Majaliwa alisema nia ya serikali si kuzuia fursa ya wakulima kuuza mahindi nje ya nchi, bali inataka kuhakikisha kila eneo nchini linakuwa na chakula, kwani baadhi ya maeneo nchini hayana chakula kutokana na kukosa mvua na hivyo kukumbwa na ukame.

Lakini, kama ni lazima kuuza chakula nje ya nchi, basi ni vema kibali kikatolewa na Waziri mwenye dhamana kwa kuuza unga badala ya mahindi. Alisema mazao yakisindikwa, yakichakatwa, yakabanguliwa na yakikobolewa kama vile mahindi, viwanda vya kukoboa na kusaga vitapata kipato, watu watapata ajira na mabaki yake yaani pumba yatatumika kulisha mifugo, kuliko kama yangeuzwa mahindi, kwani viwanda visingepata kazi, vijana wasingepata ajira na mifugo isingepata chakula.

`Mchwa’ ushirika Waziri Mkuu alisema Serikali haitamsamehe mtu yeyote, atakayejihusisha na ubadhirifu wa mali za fedha za Ushirika nchini. Alisema miongoni mwa changamoto zinazoukabili Ushirika nchini ni wizi na ubadhirifu wa rasilimali za Ushirika, unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waaminifu.

Waziri Mkuu alisema changamoto nyingine ni baadhi ya viongozi wa vyama vya Ushirika, kutoheshimu miongozo ya vyama vyao na kujifanyia mambo kwa maslahi yao binafsi.

Akizungumzia dhamira ya serikali katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema itaendelea kutimiza wajibu wake na kuweka mazingira rafiki ya kustawisha Ushirika nchini ili kutoa fursa ya Ushirika kushamiri na kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi yao.

“Haikubaliki hata kidogo kuona sekta hii inayosadifu maisha ya mwafrika hamnufaishi ipasavyo, hivyo naelekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini ihakikishe kuwa vyama vya Ushirika vinaendeshwa kisayansi na kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Pia alizielekeza Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya nchini, ziingize ajenda ya maendeleo ya ushirika kama moja ya ajenda muhimu inayopaswa kujadiliwa na kuwekewa maazimio ya utekelezaji.

Pia wawe na takwimu za vyama vya Ushirika na Wanaushirika. Waziri Mkuu alisema Serikali inasafisha uozo katika vyama vya ushirika, akitaja kuwa ilianza na Chama cha Ushirika wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCO), ikaenda kwenye korosho mkoani Mtwara, sasa itaendelea kwenye kahawa, pamba na chai na amesikia kwamba Lushoto viongozi wanagombana kila

SOURCE: HABARI LEO