Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:44 am

NEWS: MAJALIWA: HAKUNA ATAKAYEKOSA DAWA

LINDI : WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba hakuna mgonjwa atakayekwenda kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati bila ya kupatiwa dawa.

Aliyasema hayo jana jioni wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Wilaya.Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe, Mama Mary katika ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi, alisema serikali haitaki kusikia wananchi wanakwenda hospitali, Vituo vya afya au zahanati na kukosa dawa.

Alisema moja kati ya ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kila mwezi halmashauri zote nchini zinapelekewa fedha za ununuzi wa dawa.

“Serikali hii ya Rais Dk John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa kila mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika hospitali yetu, mkuu wa wilaya kafuatilie huko halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa,” alisema Majaliwa kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa jana na ofisi yake.

Katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya Sh bilioni 236 zimetengwa kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017, iliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015/2016.

Zambi alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Februari 2017, Mkoa wa Lindi ulipokea Sh milioni 538 kwa ajili ya ununuzi wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD). “Hospitali ya mkoa ilipokea shilingi 195,328,186 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na pia ilitumia shilingi 127,171,700 kutoka fedha za uchangiaji kwa ununuzi wa dawa,” alieleza

source : habarileo