Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:41 am

NEWS: MAITI ZAIDAIWA KUOKOTWA KILA WIKI UFUKWENI COCO BEACH.

DAR ES SALAAM: Maiti za wanaume watatu zimekutwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach ambapo kati ya hizo moja imekutwa na jiwe kubwa lililofungwa na kamba.

Wafanyabiashara wa mihogo wa eneo hilo wamesema juzi wakiwa kwenye biashara zao asubuhi ghafla waliona maiti moja ikielea karibu na miti aina ya mikoko ikiwa na jiwe lililofungwa kifuani huku mikono yake ikifungwa na kamba.

Mmoja wa wafanyabiashara, Aziza Ally amesema baada ya kuona maiti hiyo walitoa taarifa polisi ambapo walifika saa 4 asubuhi na kuichukua kwenye gari lao.

Amesema ilipofika saa 8 mchana waliona maiti mbili kila moja ikiwa kwenye kiroba zikielea ndipo mmoja wao alitoa taarifa polisi baadaye zilichukuliwa.

"Polisi walipokuja kuchukua hizi maiti hakuna hata mtu mmoja aliyeruhusiwa kusogelea na kupiga picha tulishangaa sana kuona jana ulinzi mkali tofauti na siku zote na aliyebainika amepiga alipokonywa simu yake," amesema Ally.

Mfanyabiashara mwingine Issa Isaya amesema cha kushangaza maiti zinazookotwa ni za kiume pekee hivyo wanaishi kwa wasiwasi kwa kuwa kila wiki wanakuta maiti zikiwa zinaelea kwenye maeneo hayo.

Amesema Septemba 20 mwaka huu maeneo hayo iliokotwa maiti ya kiume iliyofungwa kwenye kiroba ambayo ilikuwa imeharibika .

Isaya amesema maiti hiyo iligunduliwa na wavuvi waliokuwa wanavua samaki ambao huwa wanatoa taarifa kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Amesema mwanzo alikuwa anapata shida alipokuwa anaona maiti katika eneo hilo hivyo kwa kuwa kila wiki wanaokota maiti amelazimika kuizoea hali hiyo.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne amesema tukio hilo atazungumzia Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Alipotafutwa Kamanda Mambosasa amesema hajapata taarifa ya kuokotwa maiti hizo hivyo anafanyia uchunguzi na atalitolea ufafanuzi leo.

#mwananchi.