- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAHAKAMA YATAKA KUJUA AFYA YA LISSU
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam imewataka wadhamini wa aliyekuwa Rais wa TLS na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwenda na uthibitisho wa maendeleo ya afya yake pindi kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 baada ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba kuuliza maendeleo ya Lissu na mdhamini wa mwanasheria mkuu huyo wa Chadema, Robert Katula kudai kuwa Lissu bado anaumwa.
Leo mahakamani baada ya maelezo ya mdhamini wa Lissu, wakili wa Serikali, Estazia Wilson alieleza kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, hawawezi kuendelea na watamsubiri Lissu hadi afya yake itakapoimarika.
Baada ya maelezo hayo hakimu Simba amesema shauri hilo litakapotajwa tena mahakamani hapo mdhamini wa Lissu anatakiwa kuja na uthibitisho wa maendeleo ya mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.
"Mdhamini wa Lissu utatuletea uthibitisho wa afya ya Lissu ili tuweze kuweka kwenye rekodi zetu," amesema Simba na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21, 2019.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Lissu na wenzake watatu wa Gazeti la MAWIO wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti ya mwaka 2002.
Septemba 7, 2017 Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.
Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kukamilisha matibabu.