Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:39 am

NEWS: MAHAKAMA YAMUACHILIA HURU MKURUGEZI WA TBC

Dar es Salaam: Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya mahakama hiyo kumkuta hana hatia

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 25, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha mashtaka yake. Tido alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza Januari 26, 2018, kujibu mashtaka matano. Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7/2018, Tido alikabiliwa na mashtaka matano, mashtaka manne ni ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni. Agosti 27, 2018 Mahakama hiyo ilimkuta Tido na kesi ya kujibu baada ya Hakimu Shaidi kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka.

Baada ya Tido kukutwa na kesi ya kujibu, alianza kujitetea. Katika utetezi wake, Tido alidai kuwa mchakato mzima wa kuingia ubia wa kuhamisha TBC kutoka katika mfumo wa analojia kwenda digitali ulifanywa na bodi ya TBC. Akihojiwa na wakili wa Takukuru alidai kuwa hakuna kitu alichokifanya bila ridhaa ya bodi na bodi ndiyo iliyomuagiza afanye mchakato wa awali na ulipokamilika aliwasilisha kwao, mwaka 2009. Alidai kwamba hadi anaondoka TBC hakuna mtu yeyote aliyezungumzia suala hilo, si Serikali wala bodi.