Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 8:45 am

NEWS: MAHAKAMA YAKUBALI KUTOWAFUTIA DHAMANA WABUNGE CHADEMA

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali utetezi wa wabunge wanne wa Chadema wa kutowafutia Dhamana ambayo hakimu alidai walikiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila taarifa yoyote na kuwaonya vikali iwapo watarudia tena.

Onyo hilo limetolewa leo Jumatano Novemba 20, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kusikiliza utetezi wao, kubainisha kuwa haukujitosheleza lakini hatowafutia dhamana kwa kuwa itakuwa hatua kali.

Novemba 15, 2019 mahakama hiyo iliamuru wabunge hao, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Heche (Tarime Vijijini); Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda) kukamatwa baada ya siku hiyo kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Mbali na kutoa amri hiyo, mahakama hiyo pia ilitoa hati ya wito kwa wadhamini wao kujieleza kwa nini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani.

Wabunge hao walianza kujisalimisha kuanzia Jumamosi iliyopita na leo mahakama hiyo ilipanga kutoa uamuzi kuhusu kukiuka kwao dhamana.

Wabunge hao pamoja na wenzao watano akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Akitoa uamuzi huo Hakimu Simba amesema maelezo yaliyotolewa na washtakiwa hao pamoja na wadhamini wao hayajitoshelezi lakini kuwafutia dhamana ni hatua kali.

Amesema washtakiwa hao kujisalimisha polisi walikuwa wakiogopa kitakachowapata.

Ijumaa iliyopita Mbowe, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na Esther Matiko (Tarime Mjini) ndio waliofika mahakamani kusikiliza kesi hiyo.