Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 8:08 pm

NEWS: MAHAKAMA KUU YA KENYA YAPIGA MARUFUKU USAJILI WA ALAMA ZA VIDOLE

Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa agizo la kusitishwa kwa mchakato wa mfumo wa usajili wananchi kwa njia ya alama za vidole hadi hapo sheria ya kulinda taarifa itakapopitishwa.

Mbali na kuzuia utekelezaji huo, mahakama imesema kuwa kukusanya taarifa za eneo (GPS) na vinasaba (DNA) ni kinyume na katiba ya nchi.

Serikali ya Kenya imekuwa ikikusanya taarifa mbalimbali katika usajili huo ikiwa ni pamoja na alama za vidole, taarifa za familia, na eneo kamili mtu analoishi.

Wakati wa zoezi hilo ambalo serikali ilisema ni la lazima wale wote ambao hawatojiandikisha hawatopata huduma za msingi za serikali kama vile pasi ya kusafiria (passport), na cheti cha kuzaliwa.

Mahakama imezuia zoezi hilo kwa kile ilichoeleza kwamba wananchi wanaweza kujikuta katika hatari isiyorekebishika endapo taarifa zilizokusanywa zitatumiwa vibaya.

Majaji watatu wa mahakama hiyo waliamuru kusitishwa kwa mpango huo unaofahamika kama Huduma Namba hadi sheria ya kina ya kulinda taarifa zinazotolewa na wananchi upitishwe.