Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 8:36 am

NEWS: MAHAKAMA KUTOA UWAMUZI DHAMANA YA WABUNGE 4 WA CHADEMA

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Jumatano Novemba 20, 2019 imepanga kutoa uamuzi dhidi ya wabunge wanne wa Chadema waliokiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila taarifa yoyote kutoka kwao wala wadhamini wao.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 19, 2019 na hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea kwa nini wasifutiwe dhamana baada ya kukiuka masharti.

Ijumaa iliyopita Novemba 15, 2019 mahakama hiyo iliamuru wabunge hao, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Heche (Tarime Vijijini); Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda) kukamatwa baada ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Mbali na kutoa amri hiyo, mahakama hiyo pia ilitoa hati ya wito kwa wadhamini wao kujieleza kwa nini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani.

Wabunge hao wamerudishwa mahabusu na kutakiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho saa 4:30 asubuhi ili mahakama hiyo itoe uamuzi.

Amri ya kukamatwa ilitolewa na Hakimu Simba baada ya washtakiwa hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.

Leo aliyeanza kujitetea ni Mchungaji Msigwa aliyedai kuwa alichelewa mahakamani baada ya gari alilokuwa akisafiria akiwa pamoja na Heche kupata ajali eneo la Dar Freemarket.

Amesema walilazimika kutumia usafiri wa pikipiki hadi mahakamani lakini walikuta kesi yao imeahirishwa.

"Hakimu naomba usinifutie dhamana kwa sina rekodi mbaya ya kuidharau mahakama,” amedai Msigwa.