Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:26 pm

NEWS: MAHAKAM YAIAGIZA JAMHURI KUHARAKISHA UPELELEZI KESI TITO MAGOTI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, leo Februari 19, 2020 imeuagiza upande wa Jamhuri kueleza bayana hatua iliyofikiwa kwenye upelelezi wa kesi inayomkabili, Mfanyakazi wa kituoa cha haki za Binaamu nchini Tanzania (LHRC) Tito Magoti na Mwenzake Theodory Giyani, badala ya Kusema kuwa Upelelezi Bado haujakamilika au Upelelezi Umefikia Hatua nzuri.

Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyani, wanakabiliwa na mashtaka matatu, ikiwemo utakatishaji wa pesa kiasi cha shilingi milioni 17, kushiriki genge la uhalifu pamoja na kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa kwa ajili ya kufanya uhalifu.

Kesi hiyo leo ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa

Wakili wa Serikali Mkuu Monica Mbogo, Februari 5 mwaka huu alisema kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Afisa huyo bado haujakamilika kwani bado unahitajika ushahidi mwingine kutoka nje ya nchi, sasa leo Wakali huyo amesema upelelezi bado haujakamilika ndipo Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Janeth Mtega akauwagiza upande wa Mashitaka kuharakisha Upelelezi huo.

Tito Magoti alikamatwa na watu wasiojulikana mnamo Desemba 20, 2019 akiwa eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam na kutokomea naye mahali pasipofahamika, hali ambayo ilizua taharuki na kuibua hali ya sintofahamu miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu nchini na ya kimataifa ambayo yalishinikiza watekaji hao kumuachia Tito Magoti pamoja na mwenzake mara moja.

Hata hivyo, tukio la kutekwa kwa Tito na mwenzake lilionekana kuwa na mvutano baada ya kamanda wa kanda maalum ya Dar es Salaam na kamanda wa mkoa wa kipolisi kinondoni kutoa taarifa zinazokinzana kuhusu kushikiliwa kwa Tito Magoti na Theodory Giyan.

Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, kabla ya kufikishwa mahakamani walishikiliwa kwa zaidi ya masaa 72 huku taarifa za kukamatwa kwao zikiwa hazijawekwa wazi kinyume na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mnamo Disemba 24, 2019 Tito Magoti na mwenzake walifikishwa mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria za Tanzania.