Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 11:57 pm

NEWS: MAHABUSU KEKO APATIWA DHAMANA KWA NJIA YA KIMTANDAO

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania leo Januari 14, 2020 kwa mara ya kwanza imetoa dhamana kwa Mahabusu Abubakari Seguni alikuwa katika Gereza la Keko kwa njia ya Kimtandao maarufu kama ‘Video Conference’ ambaye aliyekuwa akikabiliwa na Kesi ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Dhamana hiyo imetolewa na Mahakama hiyo kwa kushirikiana na Gereza la Keko lilipo katika jiji hilo, wakati ilipokuwa ikiendesha mashauri nane (8) kwa njia ya hiyo ikiwa ni mwendelezo.

Mtuhumiwa huyo namba tatu ambaye anakabiliwa na tuhuma ya rushwa na uhujumu uchumi katika shauri namba 43 la mwaka 2017 la jinai, akiwa na wenzake watano dhidi ya Serikali. Shauri hilo liletwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Awali Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali, Bi. Ester Martin alidai kuwa shauri hilo halijakamilika kwa sababu upelelezi wake haujakamilika na linasubiri kibali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Akisoma masharti ya dhamana mahabusu huyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Augustina Mmbando alieleza dhamana ya mshitakiwa ipo wazi kwa kuwa na wadhamini wawili watakao weka ahadi ya shilingi milioni Sitini (ml. 60) na mmoja kati yao lazima awe mtumishi wa Umma na kwa pamoja wawasilishe mahakamani hati zao za kusafiria.

Akiahirisha shauri hilo, Mhe. Mmbando alisema litatajwa tena Januari 2, mwaka huu saa tatu kamili asubuhi.

Mashauri mengine saba ya jinai yaliyosikilizwa kwa njia hiyo, ambayo yako katika hatua ya awali ya kutajwa yote yalihusu Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kama inavyoelekeza Sheria Namba Tatu ya mwaka 2016 iliyofanya mabadiliko ya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura namba 200, ambayo upelelezi wake haujakamilika na mengine yakisubiri kibali kutoka kwa DPP.

Ambapo shauri la kwanza lilikuwa linamhusu mtuhumiwa Eke Bidi dhidi ya Serikali, watuhumiwa wengine ni Wolfgang Sylivester, Xiao Shaudan, Hariri Hariri na wenzake, Mohamed Ismail Sued na wenzake, Ally Anguzuu Sharifu na wenzake, Maarifa Abbas Nassor na wenzake na Mohamed Mohamed, wakiwemo wenzake watano wote dhidi ya serikali.

Mashauri hayo yote yatatajwa tena Januari 27, mwaka huu.

Mmoja wa wananchi waliofika mahakamani hapo kusikiliza shauri la ndugu yake, Bw. Rajabu Bakari mkazi wa Kongowe alisema teknolojia ya Mahakama Mtandao ni nzuri ila angependa kumwona ndugu yake uso kwa uso.

Mashauri hayo yenye mahabusu 24 yameendendeshwa mahakamani hapo kupitia gereza hilo kufikia 10, ambapo mawili yaliendeshwa wiki iliyopita Januari 10, mwaka huu.

Uendeshaji wa mashauri kwa njia hiyo ni mojawapo ya malengo ya Mahakama ya Tanzania ya kuweza kusikiliza mashauri kwa wakati na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri hayo mfano kuwalipa mashahidi, kuwasafirisha mahabusu, usalama wa mahabusu , zikiwemo nyingine.