Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:46 am

NEWS: MAGUFULI AMWAGA NEEMA KWA VIJANA.

DODOMA: Serikali imetangaza neema ya ajira kwa vijana wenye shahada ya kwanza, waliohitimu mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa maarufu kama ‘Oparesheni Magufuli.

Hayo yamebainishwa leo na Katibu mkuu ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Dk. Laurean Ndumbaro, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake jijini Dodoma.

Dk. Ndumbaro, amesema kuwa vijana wote walioshiriki katika oparesheni mbalimbali nchini na wamelitumikia jeshi la kujenda taifa (Jkt) kwa zaidi ya miaka miwili wenye sifa hizo wanatakiwa kupeleka wasifu wao (CV), pamoja na vyeti ili wapate ajira katika utumishi wa Umma.

“Ndugu waandishi wa habari kama mnavyofahamu kuwa Rais, alitoa maagizo kuhusu vijana hawa wa oparesheni Magufuli, ambao wametumikIa jeshi la kujenga Taifa kwa zaidi ya miaka miwili waajiliwe sasa kupitia kwenu nawatangazia wote wenye sifa walete CV, zao pamoja na uthibitisho mwingine ili waweze kupata ajira katika utumishi wa umma”amesema Dk.Ndumbaro.

Aidha amesema baada ya kuhitimu mafunzo hayo wapo baadhi ya vijana ambao wameamua kujitolea na kuendelea kufanya kazi kwenye makambi mbalimbali ya jeshi la kujenga Taifa(Jkt) kwa moyo na kwa kujitolea.

“Kwa kutambua mchango wa vijana ambao wamekuwa wakijitolea na hawajapata ajira hadi sasa, Rais wa Jamhuri ya Muunhgano wa Tanzania Dk. John Magufuli ameelekeza vijana wote wenye shahada ya kwanza waliohudhuria na kuhitimu ‘Oparesheni Magufuli’ ambao wamejitolea kufanya kazi za katika jeshi la kujenga Taifa (Jkt) kwa kipindi cha miaka miwili wapewe ajira”amesema.

Dk. Ndumbaro alisema kuwa vijana hao wanaelekezwa kuwasilisha Taarifa binafsi (CV), vyeti vya elimu,Taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jkt vilivyothibitishwa na Jkt, katika ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora ili serikali iweze kuona namna ya kuwatumia vijana hawa katika maeneo mbalimbali serikalini”alisema Dk. Ndumbaro.

Kuhusu vyeti feki

Akizungumzia suala la usimamizi wa Rasilimali na Mishara na uhakiki kwa vyeti vya watumishi wa Umma amesema pamekuwepo na udanganyifu na upendeleo wa baadhi ya waajiri kwenye upandishwaji wa vyeo na kuongeza wimbi la utapeli.

Aidha alisema kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora imebaini kuwa kuna waajiri wanaowasilisha katika ofisi yake taarifa za uongo kuhusu upandishwaji vyeo kwa watumishi kwa nia ovu.

Amesema taarifa hizo zinatumwa na waajiri zikitaka watumishi wao wapandishwe vyeo bila kutimiza vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazo simamia utumishi wa umma.

Hatahivyo aliwaonyoa viongozi pamoja na wakuu wa taasisi za umma ambao wamekuwa wakijihusisha na tabia hizo kuacha mara moja kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.