- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAGUFULI AIPA KIBANO BARRICK
DAR ES SALAAM: RAIS John Magufuli amesema ataifunga migodi ya madini nchini, iwapo wawekezaji watachelewa kufanya mazungumzo ya kurejesha fedha walizochuka kutokana na udanganyifu walioufanya katika kusafi risha nje mchanga wa madini maarufu makinikia.
Alisema hayo alipozungumza wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 50 ya kiwango cha lami kutoka Nyakanazi wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera hadi Kakonko mkoani Kigoma.
Alisema anasubiri wawekezaji hao waje kwenye mazungumzo, lakini kwamba muda ukizidi, mazungumzo hayatakuwepo na migodi itafungwa. Rais Magufuli alisema nchi imechezewa vya kutosha; na umefika wakati sasa wa kupambana kuondoa mafisadi na kupigana vita ya uchumi, ambayo alikumbushia tena kuwa ni vita ngumu inayohitaji mapambano ya kweli.
“Ndio maana nasema kama kuna baya lolote linitokee, mimi nimeamua kupambana kwa ajili ya watanzania, nafahamu Mungu ni mwema na Watanzania ni wema watasimama, lakini lazima hawa waliozoea kufanya nchi shamba la bibi washindwe,”alisema Rais Magufuli.
Alisema ametoa nafasi kwa kampuni hiyo ya Barrick kufanya mazungumzo na viongozi na wataalamu wa Tanzania, kuona jinsi ya kupitia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Maalumu ya Pili iliyoundwa kuchunguza masuala la kisheria na hasara ya kiuchumi iliyopatikana.
Alisema kama wawekezaji hao wataendelea kuvuta muda, ataamua kufunga migodi yote. “Tumekaribisha mazungumzo na kama wakichelewa, nitafunga migodi yote, nitaamua kuwapa wananchi wachimbe ili walipe kodi, hatuwezi kuendelea kuchezewa, kama hizo hela za madini zingekuwa zinatolewa ipasavyo hata nyie wananchi wa Kakonko mngekuwa mnakunywa chai na mikate kama Watanzania wengine,”alisema Rais Magufuli.
Alisisitiza kuwa ni bora migodi igawanywe kwa Watanzania wazalendo wachimbe wenyewe wauze na kulipa kodi kuliko kuruhusu wawekezaji `wezi’. Alisema wamekuja wawekezaji wakachimba madini na kuwaibia Watanzania kwa muda mrefu ; na wanadai wanachobeba ni mchanga, wakati kuna aina 12 za madini zilizokuwa zikisafirishwa bila kulipiwa kodi.
Alielezea kushangazwa na baadhi ya Watanzania wachache wasaliti, wanaopinga juhudi zinazofanywa na serikali. Aliwafananisha watu hao na ‘Mawakala wa Shetani’. Alisema watu hao wanataka kuwaona Watanzania wakiendelea kuwa masikini, jambo ambalo serikali yake haitakubali kuona likiendelea.
“Madhahabu yote yale yangekuwepo, kulikuwa hakuna haya ya kulalamika chakula hapa, fedha zilisombwa, ndio maana nasema kwenye vita ya uchumi lazima tusimame wote pamoja bila kujali vyama vyetu,” alisema Rais Magufuli.
Aidha aliwapongeza wabunge wote walioungana kutetea hoja na kuhakikisha sheria kandamizi ya madini inabadilishwa kwa maslahi ya taifa na watu wake. Rais Magufuli aliendelea kusema kuwa amekuwepo serikalini kwa muda anajua mambo mengi yanayofanyika, ambayo watanzania wengi wakijua watalia, kwani fedha nyingi zimesombwa na kuwaacha watanzania kuendelea kuwa masikini.
Alisema hiyo ni vita ya uchumi na kwamba Watanzania hawana budi kusimama pamoja naye kumuunga mkono katika jitihada za kuwatetea Watanzania, kwani shida za eneo hilo ni za Watanzania wote, hivyo ni vyema kuzitatua kwa ushirikiano.
Katika hilo, amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zao za kubadilisha sheria kandamizi ya madini, ambayo kwa muda mrefu iliwapa nafasi wawekezaji kubeba madini yetu bila nchi kunufaika kwa lolote. Imeandikwa na Fadhili Abdallah (Kibondo) na Ikunda Erick (Dar).
source: habarileo