Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 12:37 am

NEWS: MADEREVA WA BODABODA WATAKIWA KUFICHUA WAHALIFU.

DODOMA: MADEREVA wa Pikipiki maarufu kama bodaboda wametakiwa kuwa mabalozi wazuri katika kufichua wahalifu.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jakson silya ambaye ni Mkuu wa kituo cha polisi Kwamtoro wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa kufunga mafunzo ya udereva yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Dodoma.


Alisema madereva wa pikipiki wamekuwa wakitumia na wahalifu ni vyema wakawa mabalozi wazuri wa vyombo vya dola kufichua wahalifu.


“Lazima muwe wazalendo kwa kutoa taarifa, kataa kubeba jambazi, kataa kwenda kumficha mhalifu mna nafasi kubwa ya kufanikisha usalama, piamuangalie namna ya kufanya kazi nyakati za usiku, sio unakodiwa usiku na mtu ambaye humfahamu kwa tama ya Sh. 10,000 tu unakwenda kupotezamaisha” alisema


Alisema wako watu wengi katika tarafa ya kwa Mtoro na Farkwa ambao hawajui kuendesha pikipiki lakini wamekuwa wakifanya biashara yakubeba abiria na sasa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.


“Pamoja na kufanya kazi ya bodaboda lazima uangalie uhai wako na kujulisha wenzako umeondoka na nani na kama umekodiwa usiku sana mshawishi abiria alale ili alfajiri muwahi safari” alisema


Alisema kufanya udereva wa pikipiki bila mafunzo ni kuhatarisha maisha ya dereva na watu wengine.


“Tafiti zilizofanyika zinaonesha kujifunza ni kuongeza ujuzi wa kazi, kazi ya udereva inagusa maisha ya watu lakini sehemu kubwa yawanaofanya udereva wa pikipiki hawana ujuzi wa kutosha” alisema


Alisema kuna madereva ambao wamekuwa hawavai kofia ngumu japokuwa wanazo.


“Utakuta mtu ana helmet kaifunga kwenye pikipiki lakini haivai, ninyi mliopata mafunzo mbadilike na mkaibadilishe jamii nzima “ alisema

Kwa upande wake,Kaimu Msajili kutoka VETA- Dodoma Leonidas Mushobozi alisema mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kutoa elimu kwa vijana wote ili kupunguza ajali za barabarani.


Alisema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kuwa na mabadiliko ili kulinda nguvu kazi na kuwataka waliopata mafunzo hayo kuwa chachu yamabadiliko.


Kaimu Ofisa Tarafa wa Kwamtoro, Venancia Kitomany alisema baada ya kupata malalamiko ya muda mrefu kwa vijana kufanya kazi bila kuwa naleseni utaratibu ulifanyika na mafunzo hayo yakawafikia.


Akisoma risala ya wahitimu,Michael Tamba ambaye ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Wairo alisema mafunzo hayo yalifanyika yakijumuisha
wanafunzi 56.


“Sisi wahitimu wa mafunzo tunaomba chuo hiki kiendelee kutoa mafunzo kwa wengine ambao bado hawajapata mafunzo pia Chuo kitusimamie kwakaribu zaidi kuhusu suala la upatikanaji wa leseni.