Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:40 pm

NEWS: MAALIM SEIF AGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI ACT WAZALENDO

Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad, leo Januari 30, 2020 amechukua fomu ya kugombea uongozi wa Nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho kitaifa.

Hii ni baada ya Chama hicho kukamilisha chaguzi katika ngazi za chini.

Maalim Seif amechukua fumu hiyo leo na kurejesha fomu ambapo tangu Januari, 27 hadi 26 Februari, 2020 fumu zilianza kuchukuliwa na wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.

Maalim Seif amechukua fomu katika ofisi ndogo ya chama hicho Vuga Mjini Unguja na kukabidhiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa ACTWazalendo, Doroth Semu.

Mara tu baada ya kupewa fomu, Maalim Seif amesema sababu kuu ya kuwania nafasi hiyo inatokana na uwezo wake pamoja na uzoefu alionao wa kisiasa kwa zaidi ya miaka 25 hivi sasa.

Amesema kupitia uzoefu huo ana amini nafasi ya uenyekiti taifa ataweza kuihudumia kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Chama hicho, ambacho hivi sasa kinapanga safu zake za uongozi kwa mujibu wa katiba. "Iwapo wanachama watanipa ridhaa ya kuwa mwenyekiti, basi nitasimamia nidhamu na uwajibikaji katika chama chetu ili kujenga chama imara na kikuu cha siasa Tanzania na kuleta mabadiliko wayatakayo wananchi," amesema Maalim Seif aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa upande wake, Dorothy amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, nafasi hizo zipo wazi kwa kila anayetaka kugombea ambaye ametimiza taratibu za kikatiba ya Chama hicho.

Machi 7, 2020 utafanyika uchaguzi ngome ya wazee; Machi 8, 2020 ni uchaguzi ngome ya vijana, Machi 9, 2020 ni uchaguzi ngome ya wanawake na Machi 14, 2020 itakuwa ni uchaguzi wa chama. Nafasi zitakazogombewa ngazi ya Taifa ni kiongozi wa chama, naibu kiongozi, mwenyekiti wa Taifa, makamu mwenyekiti Taifa - Tanzania Bara na Zanzibar, katibu mkuu, wajumbe wa halmashauri kuu (nafasi 15) na wajumbe wa kamati kuu (nafasi nane) uchaguzi wa viongozi wakuu utafanyika Machi 14, 2020 ukitanguliwa na chaguzi nyingine za ngome ya wazee, ngome ya vijana na ngome ya wanawake.