Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 1:37 pm

NEWS: MAALIM SEIF AELEZEA KILICHOMKUTANISHA NA RAIS MAGUFULI

Dar es salaam. Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad leo amefichuo siri ya kwanini walikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli jana Jumanne Marchi 3, 2020 Ikulu Jijini Dar es salaam.

Seif ambaye ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Zanzibar amesema kuvurugika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 ndio haswa lengo na kusudio la kukutana na rais Magufuli.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 4, 2020 katika mahojiano yanayofanyika katika ofisi ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam

“Naomba niseme wakati nipo CUF kulipozuka mgogoro nilimwandikia Rais John Magufuli kuonana nae lakini sikupata jibu nikamwandikia barua ya ukumbusho mara tatu sikupata jibu. Bahati njema siku ya kuzindua kitabu cha Rais Mstaafu Mkapa alikuja kunisalimia akanambia"

"nimesikia unanitafuta hivyo jana asubuhi nikapata simu kutoka kwa katibu wake kuwa Rais anataka muonane saa 3:30 asubuhi. Nilifika akanambia nilisikia upo Dar nikaona hakuna ya hajakupanga siku nyingine ukiwa Zanzibar nimeona nitumie fursa hii kuonana na wewe na mimi"

"nikaona hii fursa adhimu nizungumze yote yaliyo moyoni mwangu” Mshauri ACT-Wazalendo, Maalim Seif"

Jana katika kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kuibua matumaini mapya ya maridhiano, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa vyama vya upinzani Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kuhimiza haja ya kudumisha amani, usalama na upendo. Viongozi waliokutana na Rais kwa nyakati tofauti ni Maalim Seif, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Katika maelezo yake leo, Maalim Seif amesema alipata fursa ya kuitwa Ikulu baada ya kuandika barua tatu za maombi. “Kwanza ni suala zima la Zanzibar hali inakoelekea.

"Unajua kuna matatizo na mengine ni ya kihistoria lakini matatizo yale yalifika mahali mpaka watu hawasalimiani, watu hawazikani hata ndugu kwa ndugu. Bahati njema, Rais Karume (Aman Abeid- Rais mstaafu wa Zanzibar) alifikia hatua alisema hatuwezi kuendelea hivi,” amesema Maalim Seif.

"Amebainisha kuwa alianza kwa kukutana na Rais Karume mwaka 2010 na kukubaliana kufikia mwafaka uliozaa Serikali ya mseto. “Tukasema hili suala la maridhiano siyo suala la Maalim Seif na Karume, tukalipeleka Baraza la Wawakilishi na wote CCM na CUF wakakubali.

Tukasema haitoshi, wananchi wanasema nini, tukapeleka kwenye kura ya wananchi asilimia 66 wakataka maridhiano,” amesema. Hata hivyo, amesema licha ya makubaliano hayo mambo yaliharibika ulipofika uchaguzi wa mwaka 2015.

“Tukafanya vizuri sana hasa mwanzo, lakini mwisho mambo yaka deteriorate (kuzorota), hasa wakati wa uchaguzi, basi tukaona maelewano yanapotea. Tukaingia uchaguzi wa 2015 shwari kabisa bahati nzuri CCM tukawashinda. Pale ndiyo yakaanza matatizo.”

“Tukasema CCM imekuwa senior partner na hivyo ndivyo katiba inavyosema kwa miaka mitano, imefikia wakati sasa na nyinyi muwe junior partner hamtaki, lazima mwongoze ninyi. Kwa hiyo hali ika deteriorate tunarudi kule nyuma,” amesema Maalim.

Ameongeza, “kwa hiyo dhamira yangu ilikuwa nikutane na Rais kwa sababu yeye siyo rais wa Tanganyika ni rais wa Tanzania. Yanayotokea popote Tanzania yanamhusu. Kwa hiyo mazungumzo yangu yalijikita katika hali hiyo ya hali ya Zanzibar.”