- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAALIM SEIF ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI ACT WAZALENDO
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amechaguliwa kuwa mwenyekti mpya wa chama cha ACT- Wazalendo huku Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akichaguliwa tena kwenye nafasi ya kiongozi wa chama hicho kwa mara ya pili mfululizo katika uchaguzi uliofanyika jana Machi 14, 2020.
Kwa mantiki hiyo Maalim Seif ambaye alikuwa ni mshauri mkuu wa ACT- Wazalendo hapo kabla anakuwa mwenyekiti wa pili wa chama hicho tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2014.
Maalim Seif na Zitto Kabwe walichaguliwa usiku wa kuamkia leo Jumapili Machi 15, 2020 katika mkutano mkuu wa pili wa chama hicho uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi wa viongozi wa nafasi ya uenyekiti na kiongozi wa ACT- Wazalendo.
Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi wa chama hicho, Omar Said Shabaan amesema jumla wajumbe walioshiriki mchakato huo ni 375, kura halali zilikuwa 367 na zilizoharibika nane.
" Zitto Kabwe amepata kura 276 sawa na asilimia 73.6 wakati Ismail Jussa amepata kura 91 sawa na asilimia 24.2.Maalim Seif amepata kura 337 sawa na asilimia 93.30 dhidi ya wapinzani wake," amesema.
Huku akikatizwakatizwa na kelele za wajumbe wa mkutano huo waliokuwa na shauku ya kutaka kujua matokeo hayo, Shabaan amesema Maalim Seif aliwashinda Nyangaki Shilungushela aliyepata kura nne sawa asilimia 1.10 na Yeremia Maganja kura 20 sawa asilimia 5.55.
"Kwa matokeo haya nikiwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi namtangaza kwenu Maalim Seif kuwa mwenyekiti wa ACT -Wazalendo," amesema Shabaan
Baada ya kutangazwa kwa matokeo ukumbi huo ulilipuka kwa shangwe na vigelegele kwa wajumbe kushangalia baada ya mchakato huo kukamilika usiku wa kuamkia leo Jumapili.
Uchaguzi huo unaendelea leo katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya umakamu uenyekiti wa Zanzibar na Tanzania bara ambao unatajwa kuwa na mchuano mkali, kisha kesho nafasi ya katibu mkuu.