Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:01 am

NEWS: MAABARA YA KUPASUA UBONGO YAKAMILIKA 70% DAR

Serekali imesema kuwa Maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Angio Suite) imekamilika kwa asilimia 70 na kwamba inakusudiwa kuwa uenda itaanza kutumika wakati wowote kuanzia sasa.

Hayo yamesemwa hii leo Aprili 5, 2020 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dkt. Respicious Boniface wakati Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile alipoitembelea taasisi hiyo kukagua maabara hiyo, chumba cha tiba mtandao na kukagua utoaji wa huduma katika taasisi hiyo.

Maabara hiyo ya kisasa imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 7.9 ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya Tano ikihusisha ununuzi wa mtambo kutoka Kampuni ya Siemens ya Ujerumani.

Baada ya kukagua huduma mbalimbali taasisi hiyo, Dkt Ndugulile amewaagiza wataalamu kukamilisha haraka maabara hiyo na chumba cha kutoa huduma ya tiba mtandao ili huduma ianze kupatikana Juni, mwaka huu.

“Natoa maelekezo kwamba ujenzi na usimikaji mitambo ukamilike na ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni, mgonjwa wa kwanza awe ameshahudumiwa hapa,” alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa huduma tiba mtandao, wataalamu wa MOI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) watatumika kutoa huduma kwa hospitali za mikoa na wilaya.

“Wagonjwa watakaopigwa picha za X- ray katika hospitali za mikoa au wilaya zitatumwa katika chumba cha tiba mtandao na kusomwa na wataalamu wa Muhimbili na Moi na kisha kutumwa mikoani na wagonjwa kupatiwa majibu yao,” amesema Dkt. Ndugulile.