- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: LISSU APINGWA KOMBORA TLS
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeitisha mkutano wa dharura kwa wanachama wake, kujadili hatima yao baada ya kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili ya Wanasheria nchini.
Rais wa TLS, Tundu Lissu alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba baada ya mkutano huo watatoa mapendekezo ya mkutano huo. Alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano huo. Lissu aliwataka wanasheria nchini kupigania chama hicho hicho, ambacho hivi sasa kina miaka 63 tangu kianzishwe. Alisema chama hicho kilianzishwa kabla ya Uhuru mwaka 1961 kwa lengo la kupigania uhuru wa taaluma yao.
Aliwatahadharisha wanachama wa TLS, waachane na maslahi binafsi ambayo yatakiua chama hicho. Alisema endapo Bodi hiyo ya Wanasheria itaanza, masuala yote ya usajili, nidhamu na maadili, sasa yataamuliwa na bodi hiyo, ambayo yamkini itateuliwa na waziri mwenye dhamana na masuala ya sheria. “TLS ina baraza la uongozi ambalo lingeweza kujibu haya yanayotaka kutokea, lakini ni jambo kubwa imeona iitishe kikao cha dharura cha wanachama ili tupate mawazo ya pamoja,” alisema Lissu.
Alisema wapo hapo kwa ajili ya kupigania uwepo wa chama hicho na uhuru wa taaluma ya sheria, kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mikataba ya kimataifa miaka mingi, hivyo wanachotaka ni taaluma ya sheria iwe huru ili isiingiliwe na watawala na wanasiasa. Alitoa mfano kuwa mwaka 1958 Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere alishtakiwa kwa uchochezi, lakini kwa kuwa fani ya wanasheria ilikuwa ikitetea watu wote, aliweza kutetewa na kushinda.
“Mawakili wamekuwa huru kutoa utetezi kwa watu ambao serikali haiwapendi sana kwa mfano wezi wa rasilimali, vyeti feki ama vyama vya siasa, sasa kama bodi hiyo itaanzishwa na ukitetea watu hao, itabidi bodi ifikirie itakufanya nini,” alisema Lissu. Alisema hilo likitoke, safari ya mawakili itakuwa ngumu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha hilo halitokei.
Wakati huohuo, akizungumza Dar es Salaam juzi wakati wa hafla ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma kuwapokea mawakili 248, ambao wameingizwa katika orodha ya mawakili waliopo Tanzania, Lissu alifafanua kuwa mawakili ni wasaidizi wa mahakama katika kutenda haki Kwamba mawakili wanatakiwa kuielekeza jamii njia ya utawala wa sheria, haki za binadamu na demokrasia.
Alisema licha ya tishio la kufutwa kwa chama hicho, mawakili wanatakiwa kuongeza nguvu kuokoa chama hicho. Lissu alisema mawakili hao walioongezeka juzi, watafanya idadi ya mawakili nchini kufikia 6,329, hivyo huduma za kisheria zitaongezeka. “Kwa idadi ya mawakili, Tanzania ni ya pili katika Afrika Mashariki ikiongozwa na Kenya na ya mwisho Uganda.
Kuapishwa kwa mawakili hawa ni jambo jema kwani Tanzania itazidi kujipanua katika utoaji wa huduma,” alisema Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema). Kwa mujibu wa Katiba ya TLS, wanachama wa TLS ni mawakili wote wenye vyeti hai vya uwakili.
Katiba hiyo inaeleza kuwa malengo ya TLS ni kulinda na kuinua viwango vya maadili kwa wanasheria; Kuwezesha upatikanaji wa mafunzo kwa ajili ya wanataaluma ya sheria; Kupigania uhuru wa wanasheria; Kusaidia serikali na mahakama katika masuala yote yanayohusu utungaji wa sheria na utawala wa sheria nchini; Kuwakilisha, kulinda na kusaidia mawakili na jamii kwa ujumla katika masuala mbalimbali ya kisheria.