Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:35 am

NEWS: LISSU AMJIBU VIKALI PROF. KABUDI KUWATAKA WAKOSOAJI WAKAE KIMYA

MBUNGE wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, amemjia juu Waziri mpya wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi na kumwabia anapaswa kufahamu kuwa huu siyo tena wakati wa watu wa kufokewa, au kutishiwa kama watoto wa shule wa zamani “nimemsikia waziri wetu mpya wa Mambo ya Nje, akifokea na kutishia watu anaodai wanaisema vibaya na kuibagaza nchi yetu. Huyu ni profesa wa sheria, lakini anayeelekea kutokufahamu au kutoamini matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.

Lissu anasema, “kwa mujibu wa Katiba yetu, kuna tofauti kubwa kati ya Nchi na Serikali. Matendo maovu ya vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi; au ya viongozi wa serikali kama Rais, Mawaziri au Wakuu wa Mikoa na Wilaya; na au watendaji wake wengine, sio matendo ya Nchi bali ni matendo ya Serikali.”

Lissu alitoa maelezo hayo kufuatia Prof. Kabudi, kuhutubia taifa na kusema, “nchi hii iliyojengwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, siyo nchi ya kuchezewa. Siyo nchi ya kubezwa. Siyo nchi ya kudharauliwa. Siyo nchi kudhihakiwa.”

Alisema, “kama kuna Mtanzania mwenye matatizo na nchi hii, ni vema akae kimya kama yamemshinda kuyasema matatizo hayo ndani ya nchi yake.”

Prof. Kabudi alitoa kauli hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo ya uwaziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.

Alikuwa mbele ya rais, Dk. John Pombe Magufuli, Jaji mkuu, Spika wa Bunge na viongozi wengine mbalimbali, wakiwamo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Prof. Kabudi aliteuliwa na Rais Magufuli kushika nafasi hiyo, Jumatatu iliyopita. Kabla ya kushika wazifa huo, waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, alikuwa mwanadipromasia mahiri na mbobezi wa masuala ya kimataifa, mtalaamu wa utatuzi wa migogoro na jasusi aliyebobea, Dk. Augustine Philip Mahiga.

Prof. Kabudi alikuwa waziri wa katiba na sheria. Kufuatia mabadiliko hayo, Dk. Mahiga sasa ndiye waziri wa katiba na sheria.

Hata hivyo, katika hotuba yake hiyo, Prof. Kabudi hakutaja jina la mtu anayedai kuwa amekuwa akiisema vibaya nchi yake mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Lakini ni Lissu pekee kwa sasa, anayetajwa na viongozi wakuu wa serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wabunge wa chama hicho, kuwa anazunguuka mataifa mbalimbali kueleza mabaya ya serikali na kuichafua nchi mbele ya uso wa dunia.

Mbali na kumshambulia anayedai kuchafua nchi ulimwenguni, Prof. Kabudi aliwageukia nchi wahisani kwa kusema, “mwenye matatizo na Tanzania, milango iko wazi na anakaribishwa kueleza matatizo yake.”

Akaongeza, “lakini tunawakaribisha wale wanaotutakia mema.”

kijibu madai hayo, Lissu anaendelea kusisitiza, kwa mujibu wa maelezo ya Katiba, “Nchi’ ya Tanzania ni ile inayotamkwa kwenye Ibara ya 1 na 2(1) ya Katiba kuwa “… ni Jamhuri ya Muungano (inayojumuisha) … eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”

Anasema, kwa upande mwingine, serikali Tanzania imefafanuliwa katika ibara ya 6 ya Katiba. Kwamba, “… ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali za mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali yoyote.”

Akinukuu sheria hiyo kuu ya nchi, Lissu anaeleza, “kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Katiba yetu, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia; yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Siyo nchi ya chama kimoja kama ilivyokuwa zamani, kwa hiyo kuipinga au kuikosoa Serikali iliyoko madarakani sio kosa, bali ni kutekeleza matakwa ya Katiba,” anafafanua.