Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:22 pm

NEWS: LISSU AKUSUDIA KUMBURUZA SPIKA MAHAKAMANI BAADA YA KUSITISHA MSHAHARA WAKE

Dar es Salaam: Mbunge wa Singida Mashariki Kupitia chama cha Chadema, Tundu A. Lissu ameahidi kumfungulia mashtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Katibu wake wa Bunge Stephen Kagaigai iwapo watakaidi kurejesha mara moja mshahara na stahiki zake za kibunge pasina masharti yoyote.

Lissu anataka kuchukua hatua huyo mara baada ya spika huyo kusitisha mshahara na posho za kibunge za mbunge huyo tangu Januari 2019 bila kuelezwa sababu zozote za hatua hiyo na kusema anakusudia kuchukua hatua za kisheria kufikisha suala hilo, Mahakama Kuu ya Tanzania kudai haki zake.

Rais Huyo wa zamani wa TLS ametoa tamko hilo jana Jumatano Machi 13, 2019 kupitia waraka uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukizungumzia jinsi anavyonyimwa stahiki zake za msingi akiwa mbunge.

Lissu amesema tangu Septemba 7, 2017 ameshindwa kuhudhuria shughuli za kibunge kutokana na kuwa nje ya nchi baada ya kushambuliwa na risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana kisha kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.

Katika waraka huo, Lissu amezungumzia sheria na taratibu ambazo mbunge anaweza kukosa sifa ya kuwa mbunge ambazo yeye bado anazo ni pamoja na mtu kuhama chama, kuteuliwa kuwa makamu wa rais au kuchaguliwa kuwa rais. “Ninautaka uongozi wa Bunge yaani Spika Ndugai na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kurudisha mshahara wangu na posho za kibunge bila masharti yoyote,” amesema Lissu.